Tuesday, January 31, 2006

Watanzania na Ubora wa Elimu
· Je kwa mfumo huu wa elimu tutafika?


Inafurahisha pale unapoona kila mzazi ama mlezi Fulani au mtu mzima katika mazungumzo anapogusia suala la kumpeleka mtoto shule, kinyume na miaka kama 15 hivi iliyopita.
Bila shaka watanzania kwa sasa wameamka katika suala zima la elimu na ndo maana pamoja na serikali ya awamu ya tatu kujenga madarasa mengi hata kule ambako hatukutegemea bado yameonekana hayakidhi idadi ya watoto waliopo mashuleni na wale wanaoingia kila mwaka walivyo wengi.Na pindi madarasa yanapotosheleza wanafunzi huwa wengi zaidi katika darasa moja kupita uwiano wa watoto 45 kwa darasa au mkondo mmoja ambao mwalimu mhusika wa somo lolote ni rahisi kulimudu kwa hali yeyote ile.

Watanzania sasa kwa upande mwingine wanakwamishwa na hali ngumu ya kipato na umaskini kwa asilimia kubwa, vinginevyo matarajio ya sasa ya kila mwenye motto anataka amsomeshe motto huyo mpaka chuo kikuu achilia mbali uwezo binafsi wa mtoto mwenyewe.

Kwa upande mwingine katika mtazamo wa mfumo wa elimu nchini kumekuwa na madaraja ya shule kuanzia shule za awali, msingi, na hata sekondari.Katika mtazamo wangu nimeweza kuyaweka madaraja ya shule hizi kwa ngazi 3 hivi kulingana na watu wa aina gani wanaosoma katika shule gani kwa uwezo wa familia ya mtoto.Hata hivyo nakwenda kueleza kila daraja la shule kwa ufupi ila kwa kueleweka kirahisi ili wewe msomaji nisikuchoshe kwani hata hivyo yamezungumzwa mengi na kada mbalimbali za watu.

Katika shule za Tanzania kwa shule za awali na msingi, kuna shule zile za daraja la chini kabisa.Hili ni kundi la shule ambazo watoto wasomao ni wale wanaotoka familia ya watanzania walio maskini, wapatao mlo mmoja kwa siku, na tena sio mlo kamili , watanzania au familia zinazoishi chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku. Watoto hawa husoma kwenye mazingira magumu ikiwamo na upungufu wa walimu katika shule zao, walimu wasiozidi 4 kwa shule nzima. Mtakuwa shahidi nanyi wasomaji wangu katika mazingira ya shule zoote za vijijini zilivyo kwani hata madawati hayatoshi na watoto wanakaa chini.

Labda hili anaweza kuwa shahidi yule mwanachi mwenye mtoto asomae shule ya msingi Mwanyalagula wilayani Nzega, Kule Mambali wilayani Nzega, hii hali ipo na ukifika inatisha.Unajiuliza je kweli tuko kwenye utandawazi wakati watoto wanakaa chini?, hata pale shule ya msingi Idala, hii shule iko kilimita 5 tu hivi toka mjini Nzega, lakini utakuta watoto wanakaa chini,je inakuja?.Haya mimi simo,
labda ni kwa mujibu wa wananchi wenyewe katika shule hizo na si Serikali.Bado katika shule hizi ndo utakuta walimu hawazidi 4 kwa shule na kwa darasa moja wanazidi uwiano wa kawaida 45 kwa darasa, napo unategema nini katika elimu wanavyoipata kutoka kwa mwalimu huyo mmoja na tena ukizingatia hajapata mshahara kwa miezi miwili au anawaza kufuatilia mshahara nao, ni kwa mbinde kuupata.Napo mimi simo labda hawa walimu tufanye walipwe na wananchi husika katika shule hizo ili kuwapa motisha walimu.

Kundi la pili ni la shule zile za daraja la kati ambalo lina mandhari ya kuridhisha , na inaweza na kuwa na walimu wa kutosha na walimu wataalamu, watoto wanaosoma pale ni wale wanaotoka katika familia angalau wanauwezo wa kuwa na fedha za kubalisha mboga kila siku, usafiri japo baiskeli sio sekandi hand.Labda msomaji utakuwa shahidi nianposema hivi nikichukulia shule ya msingi ya Bunge iliyoko katikati ya jiji la Dar es salaamu. Hili mdilo kundi la shule za daraja la kati na mfani huu waweza kutoseleza kuelezea mfano wa shule zoote za aina hiyo katika Tanzania hii yenye mikoa 26.

Bila shaka nategemea katika shule za daraja l;a kati kuanzia mandhari ya shule, walimu, uwiano wa wanafunzi katika darasa, vitendea kazi vyote vinapatikana, na mwalimu akiambiwa anahamishia kwenye shule kama hiyo, hufurahi na huenda kwa mori woote.

Katika kundi hili huwezi kufananisha hata kidogo na kundi la awali hapo mwanzo kwa kila kigezo, ukiaznia ubora na jisi ya ufikishaji wa elimu hiyo kwa wanafunzi(ufundishaji). Utawezaje kufananisha shule kama ya Bunge na shule ya msingi ya Kinyerezi iliyoko kule Ukonga Dar es Salaamu, au shule zile nilizozitaja katika daraja la kwanza pale mwanzo?, si utakuwa hutendi haki kwa kigezo chochote kile ingawa wote wanatumia mtaala na mfumo mmoja wa elimu nchini, lakini jinsi ya upokeaji na uelewa kwa wahusika ni mdogo na hakuna kabisa kutokana na mzangira shule husika.

Lakni bado tu tunasema binadamu wote ni sawa. Usawa unakuja wapi wakati tunatofautiana kimaisha na hata elimu za watoto wetu?, Hata kwa hili mimi simo labda shirika la haki za binadamu na watalaamu wa masuala ya jamii waniambie usawa uko wapi hapa.

Isitoshe kundi la tatu na la mwisho ni la shule hizi za watu wanaoshikwa zaidi ya dola moja na nyongeza yake kwa siku, kwa mlo wao sio haba, ni mlo na kipande cha tunda, na kama sio wa kundi la kwanza kwani kwao tunda hula msimu wa matunda na ni mara moja kwa mwaka.Hili nalo ukibisha uliza mikoa inayotoa matunda mengi mara moja kwa mwaka, wanatabora mpo kwa maembe na mfano huu?.Kundi hili vile vile lia kila kitu cha kujivunia kwani hata watoto waendao shule hawajui adha ya usafiri kwenye miji kama Dar es Salaamu, kwani familia husika laweza kuwa na usafiri zaidi ya gair moja ama tatu.

Shule hizi za daraja la tatu kwa mtililiko niliouchagua ni la zile zenye gharama inayolingana ama kuzidi hata ada ya vyuo vikuu vya umma nchini, huko ndiko akina mimi, walala hoi hatuwezi kupagusa na kuthubutu kumpeleka mtoto, nitampeleka vipi wakati ada yake yaweza ktuosha kuweka kijibanda cha chuma na sebule cha kujisetiri ili kibaka asinichungulie, hata kama nitakijenga maeneo ya bonde la jangwani lisilo halali kujenga mtu.

Ni kweli kabisa shule hizi si zingine bali ni shule zile zinazoitwa ni ama Saint Fulani au Academy, kwa tafsri nisadieni jamani. Na ni kwa ukweli usiopingika shule hizi Tanzania zimekuwa nyingi kweli na kila mzazi sasa hasa wa kundi hili wanalilia kupeleka watoto waon katika shule hizi achilia mbali gharama zake.Hapa gharama huwa hawaangalii ni elimu inayoangaliwa, lakini cha ajabu hawa watu wa aina hii huisahau hata jamii walipo kwa kujali hasa watoto wao kwamba wanasoma wapi.

Hii kwa mtazamo wangu imeleta na inaleta ubaguzi Fulani na ndo gap la maskini na tajiri linapojitokeza. Lakini hata pale penye watu wasomi kama vyuoni utashangaa shule za msingi zilizo ndani ya wigo wa chuo ziko katika hali ya kundi la kwanza nililobainisha juu.Watu hawa hujali tu kwamba watoto wao wanasoma Saint ama Academy bila kuwa na huruma ya kuweka mazingira mazuri shule za wananchi wa kawaida maadamu iko ndani ya wigo wa eneo lao.

Utakubaliana nami msomaji kama utafika katika shule ya msingi Mzumbe wilyani Mvomero ambayo iko ndani kabisa na chuo hiki, yaani mabweni ya wanachuo yako jirani na shule hii, bweni kama Kibasila, Kimweri, hapo chuoni ni jirani kabisa na shule hii kiasi kwamba hata umbali wa kita hamsini haufiki.Lakini msomaji utashangaa shule ile ilivyo ndani ya wanazuo, lakini shule hii ilivyochoka huwezi ukalinganisha na mazingira iliyopo.

Mimi nilitarajia shule kama hiyo ya Mzumbe wawepo watoto wa Maprofesa, madaktari wa Falsafa na wafanyakazi wengine wenye kipato ambacho naamini kinatosha kuiwezesha shule hii ifanane na mazingira ya chuo kikuu mzumbe kwa vile iko ndani yake.Hivi kwa akili yangu huwa hamuoni aibu wanazuo nyie kama wageni wakiwatembela kutoka nje ya chuo chenu wanapotembelea sehemu mbalimabli na kuikuta shule hii?, huwa mnajitetea vipi?,ama mnaitumia mzigo serikali ya Kijiji cha Changarawe ndo mmiliki?, lakini si iko ndani yenu?.

Bila kuficha hapa kuna ubinafsi na ubaguzi kwani nina imani kuwa katika shule hii wasomao nimwale watoto wa wafanyakazi wa chini kabisa wa chuo na watoto wa wanakijiji wakati watoto wa wakubwa na wahadhri wengi waandamizi wa chuo na wengieo wanasomesha watoto wao katika shule hizi za Saint na Academy.Sawa sikatai lakini ndugu wanamzumbe si kuna watu waelewa hapo na wenye ushawishi mkubwa ndani ya serikali wengine watafiti wazuri tu ambao waweza kuomba msaada kutoka katika mashirika na serikalini na wakapata ufadhiri wa kuiboresha shule hii?, hii achilia mbali shule ya msingi Changarawe ambako nako kuna wahadhiri wanaishi jirani lakini shule nako iko katika mazingira yale yale ya Mzumbe.Jamni hii ni aibu na mimi simo cha msingi tuone aibu basi tuikarbati basi iendane na mazingira ya chuo.

Hata hivyo kwa mtazamo wangu kwa upande mwingine nakuja kuona kwamba vurugu hili la shule za aina ya tatu imekuja juu na sasa zinaleta na zinajenga gap kubwa katika jamii yetu na ndo maana Hayati baba wa Taifa aliliona hili na akaamua kutaifisha shule zoote na kuziweka serikalini, ndio kwa maana wakati ule kusingekuwa na maprofesa wa sasa, na waheshimiwa was sasa ambao hawajali hata jamii inayowazunguka kusaidia kwa kila hali hata kujenga darasa moja?, kama asingefanya uamuzi wake huo kwani nina imani kuwa wengi walikuwa wakitoka katika familia zenye kundi la kwanza nililolitaja hapo juu. Kama sio basi kataeni, lakini ukweli ndo huo.

Na kama ndivyo hivyo, watanzania na serikali kwa ujumla haioni kuna hja ya kuanza sasa kuangalia ubora wa elimu itolewayo katika shule ziszo Saint ama Academy ambako kwa imani yangu kunawafanya wenye nazo kupeleka watoto wao. Serikali hailioni hili kwamba linajenga tabaka ambalo mtoto wa hohe hahe anapata elimu wakati kwenye Saint na Academy kunatolewa elimu yenye tija?, kulikoni jamani.
Mwisho naomba kuhitimisha kwamba, cha msingi naomba pamoja na uwepo wa uelewa wa jamii wa elimu hasa kwa akina Saint na Academy, serikali nayo iimarishe sasa mfumo wa elimu uwe wenye tija kwa wanoupata, na wale wenye watoto wao katika shule za daraja la tatu basi waone aibu na wache ubinafsi wasaidie jamii kuimarisha elimu ya watoto wa walala hoi, je Mheshimiwa Margaret Sitta unalifahamu hilo?

Wednesday, January 25, 2006

Mheshimiwa Rais.J KIKWETE imarisha PUBLIC PROCUREMENT ACT(PPA-2004) na Iwezeshwe.

Public Procurement Act(2004) kwa maana ni mkataba wa sheria kama ilivyo mikataba mingine yeyote hapa nchini, ikiwa na kanuni, sheria na taratibu zake na kwa maana hiyo haina budi kuheshimiwa na kufuatwa, kinyume na hapo tutakuwa tunavunja sheria na taratibu zote na kama nijuavyo sheria yeyote ndani ya Katiba au andiko lolote lililokubalika litumike kwa mujibu wa sheria, na kwa kufanya hivyo hapana shaka mtu kuchukuliwa hatua za kisheria kama taratibu za sheria zinavyokwenda.

PPA(2004), huu ni mkataba wa sheria wa Umma wa Manunuzi na Ugavi ukipenda kuita hivyo lakini hasa kwa Manunuzi ambao uko chini ya Bodi ya Taifa ya Manunuzi na Ugavi yaani (NBMM).Mkataba huu ulianzishwa ili kusimamia taratibu za manunuzi katika Idara, Taasisi, na ofisi zote za umma nchini sanjari na kupunguza udanganyifu na ufujaji kwenye eneo hili ambalo lilikuwa likiipatia Serikali hasara kubwa kuliko eneo lolote na katika nyanja yeyote katika bajeti ya Serikali kwa Mwaka.

Kwa mfao, inakadiriwa katika Manunuzi ya Umma katika Serikali kwa mwaka 2003, Serikali ilipoteza shillingi Billion 300, zikiwa ni fedha zilizotumika na kupotea kwa ubdahirifu wa Manunuzi ya Serikali kwa vitu mbalimbali na matumizi mbalimbali za kiofisi. Kwa maana nyingine billioni 300 zilikuwa zikitosheleza katika bajeti ya wizara mbili muhimu kwa mwaka , nazo ni ELIMU NA AFYA kwa muundo wa wizara zilivyokuwa, na andhani bajeti hiyo ilikuwa hata kwa sasa ni sawa tu kutosheleza, billioni 300 ni pesa nyingi mno.
Inatosha tu kusema kwamba ukichukulia hata kwa uwiano wa kihesabu utakuta kwamba hiyo ilikuwa ni sawa na asilimia 70 ya matumizi ya serikali katika bajeti ya mwaka ikienda kwenye manunuzi.
Ukirudi kwa haraka haraka utakuta kama bajeti ya mwaka inachukuliwa kwa matumizi ya 70%, je fedha hizo ni za nani?, Jibu ni zetu sisi walipa kodi ukipenda walala hoi, ikiwa pamoja na za wahisani kwa vyovyote tutakuja kuzilipa, sasa kwa nini tusitupie macho basi katika eneo hili?, jamani Mheshimiwa rais Kikwete!.

Inatia moyo, mkataba huu wa manunuzi upo,Bodi ya kuusimamia ipo na Wizara yenye dhamana ya kumulikia kusimamia utendaji wa bodi na mkataba wenyewe ipo, sasa kinachoshindikana ni nini mpaka tunaingia kwenye ubadhirifu wa fedha zote hizo?. Kwa kweli nimetumia mfano wa rekodi za zamani kidogo lakini si zamani sana ukipenda kujua zaidi kila mwaka serikali inatumia kiasi gani katika eneo hili basi hauna budi kwenda OFISI KUU YA MKAGUZI WA MAHESABU YA SERIKALI hapo utakubaliana nami na kitu ninachokizungumza.
Mimi binafsi, wito wangu na ombi langu kuu kwa serikali ya awamu ya nne, ni kuwa ilitupie jicho kali suala hili hasa kwa kuzingatia yafuatayo;
Mosi, Bodi ya NBMM iimarishwe na iwezeshwe na si kuwepo kama kivuli na kupewa mamlaka toshelevu ya kufuatilia taratibu na uwajibikaji wa manunuzi kwa kufuata PPA 2004 katika Idara ,Taasisi na hata Mashirika yasiyo ya kiserikali lakini yako chini ya wahisani na yanasimamiwa na serikali kama vile ya DFP, kwani mashirika haya nayatumia fedha za wahisani na pengine tutazilipa kama deni.

Pili, PPA 2004, inataja ni nani anayestahili na anayetakiwa kufanya shughuli za manunuzi kwa taaluma na si kwa mazoea na uzoefu kama ilivyo sasa kuwa mtu yeyote aweza kufanya manunuzi bila ya kuzingatia kwamba hiyo ni taaluma ya watu na wanahitimu kila mwaka kutoka vyuo mbalimbali nchini.Inatosha kusema tu kwamba kutokana na mkataba huu chini ya wizara husika iiwezeshe bodi ya NBMM kufuatilia katika nyanja zoote na ofisi zoote zinazoweza kufanya manunuzi ili kubaini watu wanaofanya shughuli hizo kwamba wamesomea na wanatambuliwa na bodi, na kama wanafanya kinyume basi watolewe na kuajiriwa wapya na vijana waliohitimu katika fani hii kwani imani yangu ni kwamba wapo wengi tu mtaani.Jamani tusifanye kazi kwa kubabaisha fuateni fani mlizosomea.

Tatu,NBMM ipewe heshima na iwezeshwe kwa kupewa meno, nguvu na kwa mamlaka yoote ya kupanga, kusimamia na kutekeleza mikataba ya aina yeyote katika ngazi yeyote nchini ili mradi tu mkataba huu unahusisha kununua au utoaji huduma nyingine ambazo fedha hizo huwa kwenye kundi hili. Nasema hivyo kwa sababu katika PPA 2004 inaeleza utaalamu na Bodi ya Tenda inatakiwa kufanya nini, na nani anahusika na katika ofisi au maeneo gani.Kama vile haitoshi NBMM itambuliwe kama NBAA ilivyo kwani wenye NBAA ni wakali sana kuchezewa fani yao na mtu hauruhusiwi kufanya shughuli zao bila ya wao kumtambua ,mbona hii NBMM inachezewa hivi na haina la kusema? au tuamini kwamba ipo tu kama kivuli cha danganya toto ya wahisani wetu kama Benki ya Dunia kwamba tulitekeleza agizo lao la kuwepo mamlaka thabiti ya matumizi ya fedha za serikali katika manunuzi na ndoo maana tukainzisha na kuimarisha kwa changala macho PPA 2001?, ambayo nayo hakukizi haja na wenye taaluma yao wakastuka jinsi walivyoiandaa na kubadilishwa tena kuwa PPA 2004, lakini mbona haitelekezwi?.
Na imani kubwa kwamba kwa kutekeleza hayo na kwa mujibu wa serikali hii ya awamu ya nne, tutaweza kupunguza eneo kubwa la upotevu wa fedha zetu ambazo pengine zingelekezwa kwenye miundo mbinu mingine ili kupunguza umaskini unaotumaliza.

Mheshimiwa rais Jakaya Kikwete na timu yako hebu tupieni jicho kali PPA 2004, chini ya NBMM, ili muweze kututhibitishia ukubwa wa serikali si hoja, kinachotakiwa ni utendaji yakinifu, nawe mwenyekiti wa NBMM, Bwana Noeli Mrope amka, chachamaa huu ndo wakati wa Nguvu mpya, Ari mpya na Kasi mpya, oka jahazi la upotevu wa fedha za umma, sio siri bodi yako haina meno na inachezewa tu.
Sina makosa kwa ukweli huu,

Mtoa maoni haya ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe anasoma shahada ya kwanza ya Utawala wa Biashara katika Manunuzi na Ugavi, aliyeko Mafunzoni kwa Vitendo DSM.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Tumieni Busara na Si Mabavu,
· Juu ya maamuzi ya Maaskofu kuhusu matumizi ya Kondomu shule za Msingi


UTAWALA bora na washeria huwa pale tu maamuzi yeyote kutoka kwenye jambo lolote lenye manufaa kwa taifa linapotolewa kwa busara na si kwa mabavu.Na isitoshe maamuzi mengine si vibaya yakatoka na kusikilizwa toka kwa wananchi wa makundi mbalimbali kama watu mmoja mmoja, madhehebu ya dini na wengineo kutokana na jambo Fulani, yakatekelezwa ama kutenguliwa na serikali hata kama yalikuwa tayari yamepitishwa na serikali kwa makosa, hapa hakuna ubaya na aibu yeyote huo ndo utawala bora.

Ijulikane tu kwamba falsafa ya Ari mpya, Ngvu mpya na Kasi mpya haipo kwa maamuzi ya kibabaishaji na yasiyo na busara bila kuzingatia maoni ya wananchi kwa wingi wanasemaje, kwa kuwa si kila kinachoamuliwa na serikali kiko sahihi mia kwa mia, kama ilivyofanya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi chini ya Waziri wake mpya Mheshimiwa Magreth Sitta ,juu ya kuruhusu mtaala au muhtasari wa matumizi na kinga ya kondomu shule za msingi.

Kwangu binafsi ninazidi kuhoji na kupingana na uamuzi wa Wizara hii dhidi ya maoni yaliyotolewa na Baraza la Maaskofu la Katolic Tanzania ,kwamba wao walipinga kutumika kwa mtaala huu kwa vile unakwenda kinyume na mafundisho ya maadniko matakatifu kwa umri wa watoto hawa, kwani hata hawajui kinachoendelea katika ulimwengu wa mahusiano ya ngono.
Ingawa sipingi moja kwa moja lakini napinga yafuatayo na ninakubaliana na yafuatayo juu ya mjadala huu,

Mosi, nakubaliana na wizara hii iweke kama mada au mtaala katika somo la sayansi kama ilivyo ada na matumizi haya ya kondomu lifundishwe kuanzia darasa la angalau la sita kwani hawa ni watoto angalau wanakuwa wamekaribia kuingia uraiani kukabiliana na mikiki mikiki ya kutaka au kutakwa kwa mahusiano ya kingono.

Nasema hivi kwa sababu nin sawa tu na mada ya mfumo wa uzazi kama lilivyowekwa ifundishwe darasa la saba na si chini yake kwa imani kwamba darasa hili wanakuwa wanaelekea kwenda kwenye umri wa utu uzima au wa kuelewa kwamba kuna nini katika ulimwengu wa mapenzi.Kwa tuliosoma kupitia mtaala huo tulikuwa tukifundishwa kila kitu tufikapo darasa la saba juu ya mfumo wa uzazi, kwa mantiki hiyo kwa nini mada hii au muhtasari huu wa kondomu wasingeliuweka au ukawekwa kw watoto wa kuanzia darasa la sita?.

Pili, nakubaliana na wizara hii kuweka mtalaa huo ufundishwe kw shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza na keundelea kwa asilimia mia kwa mia na kwa ufanisi wa kabisa na si kwa kubabaisha tu ili mradi mtu kafundishwa.

Tatu napingana na wizara hii kupitisha kufundishwa kwa muhtasari wa matumizi ya kondomu shule za msingi hasa ambao wako chini ya darasa la sita kwa vile bado hawajui kinachoendelea kwa mahusiano ya ngono kwani kisingizio cha kwamba kutowafundisha eti kinasababisha kuenea kwa UKIMWI, je Ugonjwa wa malaria ambao tunaimba na kumaliza pesa mpaka kwenye makongamano mabona haujaisha kwani si hfundishwa kila nyanja?, hiyo si sababu ya msingi jamani.

Hvi fikiria motto wa darasa la kwanza anakuuliza wewe mzazi au mwalimu kama amefundishwa halafu somo halikumkaa vizuri , aulize kwamba kondomu ni nini?, je unaitumiaje?, na kwa vipi, je tutawajibu vipi hawa watoto bila ya vitendo kama mnavyowafundisha kutengeneza tiara kwenye hilo somo la sayansi au ,maumbo mbalimbali ya kihesabu. Je hili mtawafundisha kwa vitendo?, je hamjui kwamba akifundishwa akielewa atataka kutumia ili aone, tusidanganye, hapo wizara mmechemsha.

Nne, napingana na wizara hii kwa uamuzi huo wa kuendelea kufundisha matumizi ya kondomu kwa vile sijui na sina uhakika kama watakuwa wameelewana na hawa na madhehebu yoote ya dini kwa shule zao wanazomiliki wao kwamba ni lazima mtaala huo waufundishe hata wao vinginevyo hawatafundisha. Na kama hawatafundishwa watoto wote wanaosoma na watakaosoma katika shule za msingi zinazomilikiwa na madhehebu ya dini kama Romani Katoliki na kwa skondari wale waseminari, hamjui nye watu wa Wizara hii mtakuwa hamjawatendea haki watoto hawa kwa kukosa baadhi ya mtaala wa mfumo wa elimu wan chi hii kama mlivyouweka?, je mtakwenda huko kuwaamrisha wafundishe kwa kutumia vigezo gani?.

Mmh mimi macho yangu kwani hapa hakuna mshindi kwa Imani ya kuponya roho na kuikoa na si kuingamiza kwa Maaskofu dhidi ya matendo na mwili kuponya mwili na kuiangamiza roho kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, mimi simo, kwako mheshimiwa sita, sijui unaamini maandiko yapi wewe!.

Mwisho nina kila sababu za Imani,kiroho,kimatendo pamoja na kimwili kupingana kwa sababu nilizoeleza hapo juu na ninakubaliana na sababu nilizozibainisha juu, sasa ibaki kwa wana ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya ya mheshimiwa waziri Magreth Sitta kusuka au kunyoa, cha msingi tumieni busara zaidi kuliko mabavu.