Tuesday, January 31, 2006

Watanzania na Ubora wa Elimu
ยท Je kwa mfumo huu wa elimu tutafika?


Inafurahisha pale unapoona kila mzazi ama mlezi Fulani au mtu mzima katika mazungumzo anapogusia suala la kumpeleka mtoto shule, kinyume na miaka kama 15 hivi iliyopita.
Bila shaka watanzania kwa sasa wameamka katika suala zima la elimu na ndo maana pamoja na serikali ya awamu ya tatu kujenga madarasa mengi hata kule ambako hatukutegemea bado yameonekana hayakidhi idadi ya watoto waliopo mashuleni na wale wanaoingia kila mwaka walivyo wengi.Na pindi madarasa yanapotosheleza wanafunzi huwa wengi zaidi katika darasa moja kupita uwiano wa watoto 45 kwa darasa au mkondo mmoja ambao mwalimu mhusika wa somo lolote ni rahisi kulimudu kwa hali yeyote ile.

Watanzania sasa kwa upande mwingine wanakwamishwa na hali ngumu ya kipato na umaskini kwa asilimia kubwa, vinginevyo matarajio ya sasa ya kila mwenye motto anataka amsomeshe motto huyo mpaka chuo kikuu achilia mbali uwezo binafsi wa mtoto mwenyewe.

Kwa upande mwingine katika mtazamo wa mfumo wa elimu nchini kumekuwa na madaraja ya shule kuanzia shule za awali, msingi, na hata sekondari.Katika mtazamo wangu nimeweza kuyaweka madaraja ya shule hizi kwa ngazi 3 hivi kulingana na watu wa aina gani wanaosoma katika shule gani kwa uwezo wa familia ya mtoto.Hata hivyo nakwenda kueleza kila daraja la shule kwa ufupi ila kwa kueleweka kirahisi ili wewe msomaji nisikuchoshe kwani hata hivyo yamezungumzwa mengi na kada mbalimbali za watu.

Katika shule za Tanzania kwa shule za awali na msingi, kuna shule zile za daraja la chini kabisa.Hili ni kundi la shule ambazo watoto wasomao ni wale wanaotoka familia ya watanzania walio maskini, wapatao mlo mmoja kwa siku, na tena sio mlo kamili , watanzania au familia zinazoishi chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku. Watoto hawa husoma kwenye mazingira magumu ikiwamo na upungufu wa walimu katika shule zao, walimu wasiozidi 4 kwa shule nzima. Mtakuwa shahidi nanyi wasomaji wangu katika mazingira ya shule zoote za vijijini zilivyo kwani hata madawati hayatoshi na watoto wanakaa chini.

Labda hili anaweza kuwa shahidi yule mwanachi mwenye mtoto asomae shule ya msingi Mwanyalagula wilayani Nzega, Kule Mambali wilayani Nzega, hii hali ipo na ukifika inatisha.Unajiuliza je kweli tuko kwenye utandawazi wakati watoto wanakaa chini?, hata pale shule ya msingi Idala, hii shule iko kilimita 5 tu hivi toka mjini Nzega, lakini utakuta watoto wanakaa chini,je inakuja?.Haya mimi simo,
labda ni kwa mujibu wa wananchi wenyewe katika shule hizo na si Serikali.Bado katika shule hizi ndo utakuta walimu hawazidi 4 kwa shule na kwa darasa moja wanazidi uwiano wa kawaida 45 kwa darasa, napo unategema nini katika elimu wanavyoipata kutoka kwa mwalimu huyo mmoja na tena ukizingatia hajapata mshahara kwa miezi miwili au anawaza kufuatilia mshahara nao, ni kwa mbinde kuupata.Napo mimi simo labda hawa walimu tufanye walipwe na wananchi husika katika shule hizo ili kuwapa motisha walimu.

Kundi la pili ni la shule zile za daraja la kati ambalo lina mandhari ya kuridhisha , na inaweza na kuwa na walimu wa kutosha na walimu wataalamu, watoto wanaosoma pale ni wale wanaotoka katika familia angalau wanauwezo wa kuwa na fedha za kubalisha mboga kila siku, usafiri japo baiskeli sio sekandi hand.Labda msomaji utakuwa shahidi nianposema hivi nikichukulia shule ya msingi ya Bunge iliyoko katikati ya jiji la Dar es salaamu. Hili mdilo kundi la shule za daraja la kati na mfani huu waweza kutoseleza kuelezea mfano wa shule zoote za aina hiyo katika Tanzania hii yenye mikoa 26.

Bila shaka nategemea katika shule za daraja l;a kati kuanzia mandhari ya shule, walimu, uwiano wa wanafunzi katika darasa, vitendea kazi vyote vinapatikana, na mwalimu akiambiwa anahamishia kwenye shule kama hiyo, hufurahi na huenda kwa mori woote.

Katika kundi hili huwezi kufananisha hata kidogo na kundi la awali hapo mwanzo kwa kila kigezo, ukiaznia ubora na jisi ya ufikishaji wa elimu hiyo kwa wanafunzi(ufundishaji). Utawezaje kufananisha shule kama ya Bunge na shule ya msingi ya Kinyerezi iliyoko kule Ukonga Dar es Salaamu, au shule zile nilizozitaja katika daraja la kwanza pale mwanzo?, si utakuwa hutendi haki kwa kigezo chochote kile ingawa wote wanatumia mtaala na mfumo mmoja wa elimu nchini, lakini jinsi ya upokeaji na uelewa kwa wahusika ni mdogo na hakuna kabisa kutokana na mzangira shule husika.

Lakni bado tu tunasema binadamu wote ni sawa. Usawa unakuja wapi wakati tunatofautiana kimaisha na hata elimu za watoto wetu?, Hata kwa hili mimi simo labda shirika la haki za binadamu na watalaamu wa masuala ya jamii waniambie usawa uko wapi hapa.

Isitoshe kundi la tatu na la mwisho ni la shule hizi za watu wanaoshikwa zaidi ya dola moja na nyongeza yake kwa siku, kwa mlo wao sio haba, ni mlo na kipande cha tunda, na kama sio wa kundi la kwanza kwani kwao tunda hula msimu wa matunda na ni mara moja kwa mwaka.Hili nalo ukibisha uliza mikoa inayotoa matunda mengi mara moja kwa mwaka, wanatabora mpo kwa maembe na mfano huu?.Kundi hili vile vile lia kila kitu cha kujivunia kwani hata watoto waendao shule hawajui adha ya usafiri kwenye miji kama Dar es Salaamu, kwani familia husika laweza kuwa na usafiri zaidi ya gair moja ama tatu.

Shule hizi za daraja la tatu kwa mtililiko niliouchagua ni la zile zenye gharama inayolingana ama kuzidi hata ada ya vyuo vikuu vya umma nchini, huko ndiko akina mimi, walala hoi hatuwezi kupagusa na kuthubutu kumpeleka mtoto, nitampeleka vipi wakati ada yake yaweza ktuosha kuweka kijibanda cha chuma na sebule cha kujisetiri ili kibaka asinichungulie, hata kama nitakijenga maeneo ya bonde la jangwani lisilo halali kujenga mtu.

Ni kweli kabisa shule hizi si zingine bali ni shule zile zinazoitwa ni ama Saint Fulani au Academy, kwa tafsri nisadieni jamani. Na ni kwa ukweli usiopingika shule hizi Tanzania zimekuwa nyingi kweli na kila mzazi sasa hasa wa kundi hili wanalilia kupeleka watoto waon katika shule hizi achilia mbali gharama zake.Hapa gharama huwa hawaangalii ni elimu inayoangaliwa, lakini cha ajabu hawa watu wa aina hii huisahau hata jamii walipo kwa kujali hasa watoto wao kwamba wanasoma wapi.

Hii kwa mtazamo wangu imeleta na inaleta ubaguzi Fulani na ndo gap la maskini na tajiri linapojitokeza. Lakini hata pale penye watu wasomi kama vyuoni utashangaa shule za msingi zilizo ndani ya wigo wa chuo ziko katika hali ya kundi la kwanza nililobainisha juu.Watu hawa hujali tu kwamba watoto wao wanasoma Saint ama Academy bila kuwa na huruma ya kuweka mazingira mazuri shule za wananchi wa kawaida maadamu iko ndani ya wigo wa eneo lao.

Utakubaliana nami msomaji kama utafika katika shule ya msingi Mzumbe wilyani Mvomero ambayo iko ndani kabisa na chuo hiki, yaani mabweni ya wanachuo yako jirani na shule hii, bweni kama Kibasila, Kimweri, hapo chuoni ni jirani kabisa na shule hii kiasi kwamba hata umbali wa kita hamsini haufiki.Lakini msomaji utashangaa shule ile ilivyo ndani ya wanazuo, lakini shule hii ilivyochoka huwezi ukalinganisha na mazingira iliyopo.

Mimi nilitarajia shule kama hiyo ya Mzumbe wawepo watoto wa Maprofesa, madaktari wa Falsafa na wafanyakazi wengine wenye kipato ambacho naamini kinatosha kuiwezesha shule hii ifanane na mazingira ya chuo kikuu mzumbe kwa vile iko ndani yake.Hivi kwa akili yangu huwa hamuoni aibu wanazuo nyie kama wageni wakiwatembela kutoka nje ya chuo chenu wanapotembelea sehemu mbalimabli na kuikuta shule hii?, huwa mnajitetea vipi?,ama mnaitumia mzigo serikali ya Kijiji cha Changarawe ndo mmiliki?, lakini si iko ndani yenu?.

Bila kuficha hapa kuna ubinafsi na ubaguzi kwani nina imani kuwa katika shule hii wasomao nimwale watoto wa wafanyakazi wa chini kabisa wa chuo na watoto wa wanakijiji wakati watoto wa wakubwa na wahadhri wengi waandamizi wa chuo na wengieo wanasomesha watoto wao katika shule hizi za Saint na Academy.Sawa sikatai lakini ndugu wanamzumbe si kuna watu waelewa hapo na wenye ushawishi mkubwa ndani ya serikali wengine watafiti wazuri tu ambao waweza kuomba msaada kutoka katika mashirika na serikalini na wakapata ufadhiri wa kuiboresha shule hii?, hii achilia mbali shule ya msingi Changarawe ambako nako kuna wahadhiri wanaishi jirani lakini shule nako iko katika mazingira yale yale ya Mzumbe.Jamni hii ni aibu na mimi simo cha msingi tuone aibu basi tuikarbati basi iendane na mazingira ya chuo.

Hata hivyo kwa mtazamo wangu kwa upande mwingine nakuja kuona kwamba vurugu hili la shule za aina ya tatu imekuja juu na sasa zinaleta na zinajenga gap kubwa katika jamii yetu na ndo maana Hayati baba wa Taifa aliliona hili na akaamua kutaifisha shule zoote na kuziweka serikalini, ndio kwa maana wakati ule kusingekuwa na maprofesa wa sasa, na waheshimiwa was sasa ambao hawajali hata jamii inayowazunguka kusaidia kwa kila hali hata kujenga darasa moja?, kama asingefanya uamuzi wake huo kwani nina imani kuwa wengi walikuwa wakitoka katika familia zenye kundi la kwanza nililolitaja hapo juu. Kama sio basi kataeni, lakini ukweli ndo huo.

Na kama ndivyo hivyo, watanzania na serikali kwa ujumla haioni kuna hja ya kuanza sasa kuangalia ubora wa elimu itolewayo katika shule ziszo Saint ama Academy ambako kwa imani yangu kunawafanya wenye nazo kupeleka watoto wao. Serikali hailioni hili kwamba linajenga tabaka ambalo mtoto wa hohe hahe anapata elimu wakati kwenye Saint na Academy kunatolewa elimu yenye tija?, kulikoni jamani.
Mwisho naomba kuhitimisha kwamba, cha msingi naomba pamoja na uwepo wa uelewa wa jamii wa elimu hasa kwa akina Saint na Academy, serikali nayo iimarishe sasa mfumo wa elimu uwe wenye tija kwa wanoupata, na wale wenye watoto wao katika shule za daraja la tatu basi waone aibu na wache ubinafsi wasaidie jamii kuimarisha elimu ya watoto wa walala hoi, je Mheshimiwa Margaret Sitta unalifahamu hilo?

0 Comments:

Post a Comment

<< Home