Friday, February 17, 2006

MRADI WA MAJI ZIWA VICTORIA ULENGE 2050;
Ni katika kukabiliana na ukame mkali ujao
Mradi uweze kutumika kuzalisha chakula cha kutosha.


Ilikuwa ni faraja na neema kwa wakazi wote wa mikoa ya kanda ya ziwa, hasa mkoa wa shinyanga kwa kupitishwa mkakati na mradi mkubwa wa maji wa ziwa victoria, miaka kama miwili hivi iliyopita.Na nina imani mradi huo kwa sasa unaendelea chini ya wachina waliopewa ukandarasi wa kujenga.Hata hivyo si mkoa wa shinyanga pekee uliolengwa katika mradi huo, hii ilikuwa ni pamoja na mikoa ya Mwanza, Tabora na hatimae utafika mpaka makao makuu ya nchi Dodoma hata kama kwa miaka kumi na tano ijayo.

Pengine tutakumbuka, mheshimiwa waziri mkuu wa sasa, Edward Ngoyai Lowasa ndiye aliyesimama kidete bila kuteteleka na kurudi nyuma katika kuutetea mradi huu uendelee kujengwa baada ya Misri kuleta kikwazo kwamba ni wao pekee ndio wenye mamlaka ya kutumia maji ya ziwa victoria kutokana na mkataba wa kikoloni uliowaruhusu kufanya hivyo na si nchi nyingine yeyote.
Lakini hilo Lowasa hakuangalia makunyanzi ya wana wa farao, yeye akawa kama jiwe la pembeni lililowashinda waashi, basi lingewaangukia na kuwaponda na kuwasaga, huoo, mradi uliendelea mpaka sasa.
Nami nachukua fursa hii kumpongeza mheshimiwa waziri mkuu kwa kuwa shujaa kwa kiasi hicho kwa maslahi ya nchi yake.

Inatosha tu, kusema kwamba mradi huu wa maji kutoka ziwa victoria ili unufaishe wananchi woote katika sehemu ulikoanzia , kupitia mpaka utakapoishia kwa awamu, kama sikosei itakuwa awamu ya kwanza ililengwa utaishia wilaya ya Kahama mkoani shinyanga.
Mradi huu naomba ulenge hasa katika kuwezesha kilimo cha tija zaidi kwa sehemu itayonufaika na mradi huu.Mradi wa maji haya usilenge tu kama maji ya matumizi ya kawaida ya wakazi husika, kwani ni mradi ambao umetumia pesa nyingi mno za kwetu ndani na toka kwa wafadhiri nje.

Kama vile haitoshi, mradi huu ulenge ukame mkali sana ambao unasemekana utabisha hodi ifikapo 2050, pengine hata kabla ya huko kama tunavyojionea wenyewe sasa hivi.Mradi huu ukilenga mbali zaidi utatuwezesha kukuta tuna vyakula vya kutosha kwenye maghala yetu ya chakula ya kila kanda kama yapo, au maghala mahususi kwa kuhifadhi mazao mbalimbali.

Ninaonavyo mimi, hata kama shinyanga na mikoa hiyo ya kanda ya ziwa watazalisha dengu pekee, basi wazalishe dengu nyingi na za kutosha kwa kutumia mradi huu wa maji kwa kufanya kilimo cha umwagiliaji ili waweze kulisha watanzania wote ifikapo miaka hiyo ya ukame mkali 2050 kama inavyosemekana.

Nasema hivi kwa sababu, nimekutana na tafakuri ya Profesa Charles Bwenge, Mhadhiri wa Lugha katika chuo kimojawapo huko Marekani. Tafakuri yake ililenga katika upungufu wa chakula nchini.Tafakuri yake aliitoa katika gazeti mojawapo la kiswahili litolewalo mara moja kwa wiki, la tarehe 16-22, Februari 2006 katika ukurasa wa 12.

Profesa Charles Bwenge anasema "Kikundi cha watafiti nchini Uingereza kinachochunguza kuongezeka kwa joto duniani miaka minane iliyopita kilitabiri kuwa maeneo mengi barani Afrika yatakumbwa na ukame mkali sana ifikapo 2050, na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula utakaoathiri watu zaidi ya millioni thelathini(30).".Mwisho wa kumnukuu.
Binafsi mawazo ya Prof.Bwenge yaliniingia na kufikiri kwamba mwenye macho haambiwi tazama, tayari sasa joto hilo la ukame tumeanza kulionja, kwa nini tusubiri mpaka 2050?, basi napenda kuwakumbusha watanzania kutokana na hoja ya Prof. Bwenge kwamba tujiandae ipasavyo hasa kwa kuutumia mradi huu mkubwa toka ziwa victoria kama nionavyo mimi.Na tena si hivyo tu kuwepo na mpango maalumu wa kuanzisha mazao yapi yaanze na yanastahili kwa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika maeneo ya sehemu itakakopita mradi huu.

Prof.Bwenge, hata hivyo anaongeza kwa kusema kwamba, namnukuu," Ni dhahiri kuwa upungufu wa chakula ni matokeo ya mipango mibovu ya serikali katika miaka kumi, au ishirini au zaidi iliyopita, na kama hakuna hatua madhubuit zinazochukuliwa kuboresha sekta ya kilimo na techonolojia ya kuhifadhi chakula kinachozalishwa, basi huo mwaka 2050, tutakipata.Tusije kulaumu ukame"

Binafsi naungana na Prof.huyu kwa asilimia mia moja, kwani mawazo na fikra hizo zimetolewa katika muda muafaka kabisa kwa hiyo hatuna budi kujiandaa kuelekea 2050 hata kabla ya hapo, kama ilivyo sasa.
Ni muda muafaka vile vile kuanzishwa kwa mradi huu wa ziwa victoria kwani utasaidia sana katika maendeleo ya kilimo ksichotegemea msimu wa mvua sanjari na jitihada za watalaamu wa wetu wa kilimo kubaini ni mazao yapi yanastahili yapewa kipaumbele katika sehemu unakopita mradi huu, ili wananchi wa sehemu hizo wazalishe mazao hayo kwa ubora zaidi na kwa wingi zaidi kulenga 2050, kwenye ukame mkali.
Hata hivyo, niliwahi kuandika makala yangu gazeti la Mtanzania kwamba ni wakati sasa mzuri kwa watalaamu wetu wa kilimo kurudi katika fani yao ya kilimo na kwa wakulima na si kukaa maofisini tu na kutaka kufanya kazi zingine tofauti na walizosomea.
Lengo la makala hiyo ni kuwakumbusha watalaamu hawa kukiboresha kilimo chetu kilcho hoi bin taabani, ili hali tukisema kwamba eti kilimo Tanzania ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Hii ni kudanganyana, kwani tangu lini ukakuta uchumi wa nchi unategemea asilimia zaidi ya themanini(80) ya wakazi wake ni wakulima wadogo wadogo(Peasants)?, tena wakitumia jembe la mkono ukasema uchumi unatokana na kilimo cha aina hiyo?.

Kwa mantiki hii kwa nini tusisote kwa kukumbwa na ukame na jaa ya kishindo kwa vile kilimo chetu ni cha Pure subsitence farming system(Peasants), ambao wanatumia jembe la mkono katika kati ya bwawa la utandawazi na technolojia lukuki za kilimo, na mingineyo?.Au hapa hatujaligundua hili kwamba Tanzania bado tunacheza makida makida kwenye suala zima la kilimo.

Labda naomba ni jibiwe swali hili, ni asilimia ngapi Tanzania ni wakulima kwa maana ya mkulima(Farmers) na si wakulima wadogowadogo(Peasants)?,Kama wapo asilimia fulani ni kiasi gani huzalisha kutoka kwenye kilimo, na kwa nini tunasota kwa njaa sasa?.
Hapa nina uhakika hakuna jibu la moja kwa moja lakini jibu litaanzia na Inategemea.Pengine nsivuke kwenye mada yangu, ila tu nazidi kuungana mkono na Prof.Charles kwamba upungufu wa chakula nchini ni kwa sababu ya mipango mibovu ya serikali katika miaka 10 au zaidi iliyopita, na hakuna budi sasa serikali kuling'amua hilo na lianze kufanyiwa kazi mara moja.

Kama hivyo ndivyo, natoa wito na waraka wangu huu vile vile kwa serikali ya awamu ya nne ya wana Kasi mpya na wana kiwango cha kasi ya kutosha na umahiri uliobobea kuanza kuweka mipango mizuri kabisa na ya makusudi katika kilimo cha umwagiliaji wa kutumia mradi wa ziwa victoria.Vinginevyo, mradi utakuwepo na maji yatakuwepo, ila ifikapo 2050, tutakumbwa na huo ukame mkali, na njaa, halafu tutamalumu nani?.Na fikiri lawama za kwanza zitakwenda kwa woote walio kwenye dhamana ya kupanga mipango mahususi ya kilimo bora na chenye tija.Tutawalaumu hata kama watakuwa wazee wasiojiweza na wenye kutembelea mikongojo, lawama hatazikwepa.
Nasema lawama hawazikwepa kwa vila walitakiwa kuyazingatia mawazo yetu ya sasa ya mipango ya mbele kabisa na kuyapa kipaumbele zaidi katika vikao vyao mbalimbali vya taifa kama bunge au semina kama za wabunge, na wasianze na maslahi binafsi, mmh, acha nisitoneshe kidonda.

Namalizia kwa kusema kwamba, mipangi mizuri na mafanikio mazuri hupatikana pale penye nia na njia ya mipango ya mda mrefu(Long term Plan), na si papo kwa hapo.Kwa wadau, wananchi, na serikali kwa ujumla angalau yasomeni mawazo haya na myaandike kwa kalamu ya risasi, japo yatakuwa yanaonekana kwenye karatasi mlipoandika, yaweza kuja kukumbukwa na kuhitajika ifikapo kwenye kilio cha kusaga meno hapo panapotabiriwa kwenye ukame mkali 2050.

Naomba tusije rudi nyuma na kukumbuka kwamba penye miti mingi hapana wajenzi wakati tutaungana kati ya watu milioni 30 wakiugumia kwa njaa na ukame wakati tuna mradi mkubwa wa ziwa victoria.

'Sawa, kasi mpya kwenu katika kilimo cha jembe la mkono", Tusije laumu ukame na njaa ifikapo 2050.

Tuesday, February 14, 2006

OPERATION ELIMU TABORA NI LAZIMA (OETL):Yahitajika.

Wakati mkoa wa Shinyanga umeweka operation okoa Shinyanga ni Lazima, basi wana Tabora nao hawana budi kuwa na operation Elimu Tabora ni Lazima(OETL).
Mkakati wa operation ya wana shinyanga inajumuisha pamoja na kuuokoa mkoa huu kiuchumi, kielimu, kiafya na mambo mengine yanayohitasjika kuinua shinyanga kimaendeleo na maisha ya wanashinyanga.

Hata hivyo, nimeona ni bora, nami niweze kuweka waraka huu kwa wanatabora, wadau na watu wote wenye mapenzi mema na mkoa huu wa kihistoria na wazamani nchini, ambao unazidi kudorora kila kukicha na siku hadi siku katika nyanja zote mpaka kwa maisha ya wananchi wa Tabora.
Sihitaji kutaja kila nyanja na matatizo yanayoukabili mkoa huu.Kwa matatizo kwa kweli yapo mengi, lakini kutokana na mada yangu nitajikita zaidi katika operation ya elimu mkoani humo.

Mimi kama mdau,na mzaliwa wa mkoa huu huwa napata shida na inakuwa hainingii akilini mwangu kila mwaka nikisikia, kuona elimu mkoani Tabora ikishuka, kwa maana kuna mfululizo wa miaka kadhaa imepita mpaka mwaka jana Tabora inakuwa inashika nafasi ya mwisho katika matokeo ya elimu ya msingi na ikipokezana na Shinyanga, ama shinyanga ya mwisho, ikifuatiwa na Tabora ya pili toka mwisho, ama Tabora ya mwisho na Shinyanga inafuatia, vivyo hivyo, mpaka aibu na inakera kwa wazalendo wa mkoa huu.

Nasema mpaka mwaka jana kwa maana ya matokeo ya mtihani wa mwaka jana yaliyotolewa mwaka huu kwa watahiniwa wa darasa saba.Bado Tabora ya mwisho, ingawa wenye dhamana ya kusimamia elimu mkoani humo walisema mwaka huu eti Tabora elimu imepanda kwa kushika nafasi ya kumi na kitu.

Mimi sikubaliani na takwimu hizo, kwani ningelikubaliana na kupanda kwa elimu kama Tabora ningesikia wameshika nafasi ya na wako katika kumi(10) bora, kwa vile imeabika siku nyingi mno kuwa ya mwisho, ndio hapo ningeliamini kweli kweli Tabora elimu imeboreshwa na kufaulisha vya kutosha.
Na kwa mantiki hiyo kama Tabora ilijisifu kwa kupanda takwimu ya kufaulisha basi ilikuwa ikifanya hivyo ndani ya wajinga.Naamini kwamba hata kama ukichukua kundi la wajinga na kuwapa mtihami pekee, lazima apatikane aliye bora kati ya hao wajinga, na inawezekana Tabora imo ndani na ilikuwepo katika kufanya vizuri kati ya mikoa mibovu katika elimu Tanzania, hapo hatuwezi kujisifu hata kidogo.

Kuna kunashindikana nini Tabora kushika nafasi ya 1, 2 au ya 3 kitaifa ama kuwepo katika 10 bora kitaifa?.Nafikiri ndo limewapelekea wanashinyanga kuweka mkakati wa "Operation Okoa Shinyanga ni Lazima", Ili kuondokana na aibu hizi za kila kitu shinyanga ni ya mwisho wakipokezana na walina asali(Wanatabora), kweli ni aibu.
Hapa lazima tujiulize sote, ama kama wadau, wazalendo,na wasio wanatabora, kwamba kila kitu kinawezekana kama dhamira na mikakati thabiti ikiwepo juu ya jambo fulani.Kwani mikoa inayokuwa inashika 10 bora kuaznia ya 1 mpaka ya 10 ina kitu gani?,je ina mikakati ipi inayotumia mpaka kushika nafasi hizo ambazo mkoa kama wa Tabora hawawezi kutumia mikakati hiyo na kujifunza ili kuinua Elimu mkoani Tabora?, je nani alaumiwe?.

Mwaka 2004, jumamosi ya tarehe na mwezi nisiokumbuka, nilimuuliza swali mojawapo mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Nzega, Lucas Seleli, katika mkutano alipotembelea kijijini kwetu Idala ambapo ni umbali wa Kilomita 6 hivi toka Nzega mjini.
Nilimuuliza swali kwamba"Je, yeye kama mmoja wa wabunge wa mkoa wa Tabora, wana mikakati gani kuinua mkoa wa Tabora kielimu kuondokana na adha ya kuodorora kwake?, Ama je yeye kama Mbunge, huwa hawaoni aibu bungeni wanaposikia na kutangazwa kwamba mkoa wa Tabora umeshika nafasi ya mwisho?".

Nakumbuka jibu alilonijibu mheshimiwa Seleli wakati wa kujibu maswali yaliyoulizwa, ni kwamba moja alijibu kuwa ni kweli walikuwa wakipata aibu kubwa kweli kutoka kwa wenzao ambao mikoa yao inapeta kwa kuwemo kwenye 10 bora.
Ila jibu la mikakati ipi walikuwa nayo kama wabunge kushughulikia elimu mkoani humo, kwa kweli sikumbuki kabisa, labda kwa vile lilikuwa si jibu toshelevu na sahihi zaidi, ingawa laweza lilikuwa mojawapo ya majibu ya kiasi cha kuwa sahihi,mimi sikumbuki hata kidogo.Kwa maana nyingine sikuridhika na majibu ya swali langu na ndo maana sikuwa na haja ya kulikumbuka.
Hawa ndo wabunge wetu, ambao ndo wangelikuwa wa kwanza na mstari wa mbele kulia na kuomba ama kuishawishi serikali kila mara na bila kukoma ili mkoa huu uwezeshwe na kuboresha elimu mkoani humu wakisaidiana na wadau mbalimbali wa Tabora kama nilivyoanisha hapo mwanzo.

Kwangu binafsi, siwalaumu wabunge pekee katika swala hili ambao naweza kuwalaumu na kusema wanawajibu pekee wa kuimarisha elimu Tabora.Isipokuwa ni wajibu wa kila mtu mzalendo na mzawa na mwenye mapenzi mema na mkoa wa Tabora, hii iwe akiishi ndani ya mkoa huu au nje ya mkoa huu ili mradi yumo katika makundi niliyoyataja ya wanatabora.

Na nina imani kwamba wapo watu wa kada mbalimbali ambao ni wazawa, wenye asili na wazalendo wa mkoa huu ambao wako nje ya mkoa huu na wana amana nzuri tu ya mali za kipesa na kifikra, wasomi na wanazuo wazuri tu, lakini wamejisahau na kuusahau mkoa wao, kana kwamba walifanya mabaya walikotoka na pengine labda walikosea kuzaliwa kule na wangezaliwa labda mikoa mingine.

Tutasemaje hapa kama kweli watu wa kada mbalimbali wapo na wanashuhudia jamii yetu inaangamia kwa ujinga na hakuna anayepata uchungu hata wa kusema kama mimi hapa, ingawa najilaumu kwa kuchelewa kukumbushana haya.Na sina uhakika kama yatawaingia wahusika popote wasomapo maoni yangu haya ama nitakuwa napiga ngoma na wakisikia lakini wasielewe na kupuuzia.

Hata hivyo tatizo ninalolifahamu mimi kwa ndugu zangu hawa wanatabora, wanatabia ya kutokujali wanakotoka.Mwanatabora akisha fika pale alipo, mfano kule Dar es salaamu sehemu kama Msasani, Oysterbay,Mbezi Beach na sehemu kama hizo kwa mikoa mingine, basi yeye huwa hakumbuki kabisa tena na hana haja na jamii anakotoka, jambo ambalo ni tofauti na jamii kama za wachaga na ndo maana kilimanjaro hapo ilipo imefikishwa na watu wake kuupenda mji wao na kupenda na kuuendeleza kwa nguvu zoote mkoa wao.

Mwanatabora yeye hufikia hata kukana kwa utambilisho wake kwamba anatokea kati ya mikoa hii ya Tabora ama Shinyanga ama Mwanza awapo katika ustaraabu mbalimbali hata kama kuna uewezekano wa kutambulika kiasili kwa kuwapo vyama mbalimbali vya kimkoa, kikanda kama ilivyo katika vyuo vikuu nchini.Walio wengi huwa hawajitambulishi katika vyama vyao vya kinyamwezi ama MWASHITA(Mwanza, Shinyanga na Tabora), na hawako tayari kushiriki katika jambo lolote ndani ya vikundi hivi, na kama nasema uongo muulizeni Mheshimiwa Mbunge wa Maswa wa sasa, John Shibuda alikuta nini katika Chama cha MWASHITA, chuoni Mzumbe pale alipoalikwa kuwa mgeni rasmi 2004 katika moja ya sherehe iliyoandaliwa na chama hiki.

Jamani hii ni tabia gani?, unasahau jamii yako, asili yako, utamaduni wako na hata lugha mama?, wewe ni mtu wa wapi?.Huu na hawa ndo wanaoitwa 'Mabukanya" kwa maana moja ya kuwa na uroho wa kipekee na ubinafsi.Kwa nini usikumbuke kwenu? nyie mna nini? hamuoni wenzenu wanavyopafagilia kwao kama akina iwe?.Aisee inatisha na hakuna mfano.
Acha nisitoke kwenye mada yangu ya leo na hili si tatizo kubwa kama mmenielewa wahusika mmenielewa ninachobwata hapa.Cha msingi ni kwamba wanatabora kuweni na moyo wa kujionesha, kujivunia na kuwa na mapenzi mema ya kukumbuka mkoa wenu katika suala zima la Elimu.

Pengine kuna haja ya kuweka makakati wa Operation Elimu Tabora ni Lazima(OETL) Kwa maana kwamba kuwa na malengo ya makusudi kabisa ya kuundeleza na kuboresha Elimu mkoani Tabora kwa njia yeyote ile na mkakati wowote ule ili mradi Elimu Tabora Tabora inapanda, Vinginevyo tutajikuta wapagazi wa mikoa mingine kwa kuwa sisi tu wajinga Kielimu.

Bado wenye elimu zao ndo watakuwa watawala ndani ya mkoa wetu hata kama panahitajika awepo mzawa kwenye nafasi hiyo,mpaka kwenye uwenyeviti wa vitongoji watu toka mikoa mingine watashika nafasi hizo kama wanatabora watabaki nyuma kielimu na kasi yenyewe ndo hiyo ya kutupa jongoo na mti wake.

Pengine tutajikuta kila mkoa una mikakati na matarajio ya kujenga chuo kikuu hata kama kwa miaka 15 ijayo lakini sisi kwa mwendo huu, wala hatuna habari.Ndio tunahangaika na elimu ya shule ya msingi tu nayo ni mbovu seuze chuo kikuu.

Ninavyoona mimi kuna haja ya wasomi wetu, matajiri wetu, mashirika ,kada mbalimbali wa mkoani Tabora ama wenye uzal;endo na mkoa huu tukae na kukubaliana kwamba , mosi tatizo ni nini katika elimu yetu Tabora, pili tufanye nini kama tutapata tatizo,tatu, tuanzie wapi na vipi katika tatizo hilo, je rasilimali zipo pamoja na wataalamu wa elimu wazalendo?, pesa? na kama havipo tuweke mikakati ipi ili kupata rasilimali(resources) hizo ili kufanikisha program yetu ya OETL, Swala kubwa ni kuwa tunataka sasa na tunaelekeza nguvu zoote kwenye kuwekeza Elimu kwa jamii yetu hakuna kitu kingine hata kama kwa miaka yapata 30 hivi potelea mbali matunda tutavuna huko mbele.
Kwa mfano tunaweza kujiuliza maswali hayo tukiwa na mikakati ya kuweka OETL kwa miaka mitano mitano kuwa kila wilaya iwe na shule ya sekondari moja ya kuaznia kidato cha 1 mpaka 6, halafu mitano mingine kila Tarafa iwe na shule ya sekondari kuanzia kidato cha 1 mpaka cha 6, na baadae hata kijiji.Na mwisho na baade tena tunaweka mipango wa miaka kumi kumi kwamba mkoa wa Tabora uwe na chuo kikuu ifikapo mwaka 2030, HILO linawezekana kwa kabisa kwa m,ipango mahususi na ya makusudi kwa ushirikiano wa pamoja.


Si hivyo tu, mipango hii iende sanjali na kuboreshaji elimu kwa ujumla kwa kusimamia elimu yetu ikiwemo kamati na tume mbalimbali zitakazoundwa kwa mujibu wa wadau woote.Kama ikibainika kuna viongozi ama mtu yeyote aliyepewa dhamana ama na sisi au na serikali akichezea elimu mkoani mwetu basi tuwe wakali na hatuna budi kumkataa kwa vile anatuletea ugonjwa mbaya wa milele wa ujinga na upumbavu wa kutokuwa na elimu bora.

Kwa mpango huu inawezekana kabisa kama wakubwa wetu wengine wakiweka hata harambee, chakula cha jioni ya mara moja hata kwa mwaka kukutana na nakuchangia mali za akili, fikra yakinifu, vifaa na pesa ili kuinua elimu mkoani mwetu.

Ndugu zangu hakuna atakayekuwa na uchungu na mkoa wetu kama sisi wenyewe hatuujali na kwa kudorora kwake katika nyanja zoote hasa kielimu kwani tukiwekeza kwanza kwenye elimu na mambo mengine yatafuata, vinginevyo tunaiweka rehani jamii yetu kuwa watumwa wa milele kwa kutokuwa na elimu bora

Naongeza tena cha msingi tuache ubinafsi, uroho wa kipekee na tamaa za kujidai kutokujali jamii yetu, huo sio ujanja ni ushamba na ujinga katika jamii iliyoelimika.
Kwani hatuoni au huwa hatusikii kutokana na mifano wa mikoa mingine unakuta wanaitishana kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwamba wana mkoa fulani wanatakiwa wakutane tarehe fulani na mahala fulani, agenda ni kujadiliana jinsi ya kutatua matatizo ya mkoa huo, moja likiwa ni elimu, na hapo hapo unasikia na mgeni rasmi atakuwa mheshimiwa fulani(Labda waziri au mkurugenzi wa kampuni fulani), kwa sisi hilo haliwezekani?, je hawa waheshimiwa sisi hatunao?, au hawatambui hilo?.

Jamani tujifunze basi kwa mifano na vitendo kama hivyo juu, kuinua elimu yetu Tabora.
Hivi nyie wenzangu tukishapita sisi ambao angalau tuna hicho kielimu au tumeshapata kidarasa bora kiasi kuliko wenzetu wa sasa na jua likatufika saa 10, hiyo jamii inayopata elimu mbovu na hakuna uwiano wa wasomi wengi mkoani humo kwa nyakati hizo nani atawasikiliza katika matatizo yao kwa vile watakuwa nyuma nusu saa kielimu kuliko mkoa wowote?.

Namalizia, jamani wasomi wetu(maprofesa wanatabora, madaktari wa falsafa wanatabora, wenye shahada za uzamili, shahada za kwanza, diploma na wenye vidato wanatabora) mko wapi kuinua elimu mkoani mwenu?, amkeni kumekuchwa, tunaachwa na gari la utandawazi wa elimu.Jamani wenye mali zenu za kipesa na maarifa wanatabora mko wapi kuchangia elimu yenu ili iboreke katika jamii ya wanatabora?, amkeni kumekuchwa, tunaachwa na gari la utandawazi wa elimu.

Jamani waheshimiwa akina Prof.Juma Kapuya, akina spika wa standards and speed, ioneshe speed yako hata mkoani kwako na jimboni kwako amabko kuansekemkan kuna umaskini usio na mfano, je unasimamia kiwango gani wakati kiwango(standards) cha elimu mkoani kwako kimedorora?, weka kiwango hicho kwa wanatabora, kila kitu kitawezekana.Jamani waheshimiwa wabunge akina Dr.Msekela, Lucas Seleli mko wapi,madiwani wetu mko wapi? wekeni mikakati kuboresha elimu ya wanajamii wa tabora, nyie ndo tumewatuma mkahemee bungeni ni pamoja na elimu bora.je na nyie wananchi je mko hange hange kwa hili la elimu au ndio mshika shuka na ngoma za waswezi na uyeyebila kujali elimu?, amkeni jamani gari la utandawazi hilooo,linapita litatuacha.

Hitimisho, "Haya jamani Kasi mpya ya kusahau kwenu", mtanikumbuka hata kama nitakuwa sipo duniani hata kwa kifikra zangu hizi".

Saturday, February 04, 2006

CHUO KIKUU KIKUU MZUMBE NA HATIMA YA MAPINDUZI YA SERIKALI(MUSO).

Ni pale tu uongozi uliopo madarakani unaposhindwa kukidhi na kutekeleza yale iliyoahidi kwa wananchi wake, ndipo wanachi wale wale hurudi na kutaka kuiondoa serikali husika kwa vile imekwenda kinyume na ilichokiahidi kwa hadhira husika.

Ilikuwa ni jumamosi ya tarehe 28, january 2006, ndipo mgogoro wa mapinduzi ya serikali ya wanafunzi Mzumbe ulipoanza na kujitokeza masikioni mwa wakazi wa wananchi wa Mzumbe chuoni pamoja na majirani zake na kesho yake taarifa zikawa zimeenea karibu nchi nzima.Mgogoro huo umeendelea mpaka siku ya wiki iliyofuata ya tarehe 3, February 2006, na kwa maana nyingine mgogoro wa kuipindua serikali iliyokuwa madarakani imechukua mda wa wiki nzima.

Hata hivyo mapinduzi hayo yalifanyika na yaliendelea kufanyika ili hali wanafunzi wakiwa wanaendelea na mitihani yao ya semista ya kwanza.Hawakuchelea pamoja na kuwa walikuwa na mzigo wa mitihani hiyo, lakini waliona bora kujikomboa kutoka uongozi mbovu uliokuwepo wa MUSO na pengine hata menejiment ya chuo.

Nasema hivi kwa sababu kuna haja gani kwa wananchi wa mzumbe kutaka kuiondoa serikali husika ndani ya mitihani ama ingelikuwa nchi kamili ni katikati ya kukuza uchumi na kwenye matatizo kama ya njaa kwani mitihani ni kama kupanda na hatimae ukavuna.
Lakini hapo waweza kuvuna au kukosa na ndo hapo hufanana na kufeli kwa maana ya mazingira ya wanachuo.Lakini hayo yoote hawakuangalia wanajumuia wa Mzumbe, wakaamua kumwondoa labda nduli wao, ili wajikomboe.

Wananchi wa Mzumbe niliwafananisha na Bwn Stephen Biko wa Afrika Kusini pale, mpigania uhuru wa afrika kusini pamoja na akina Mandela pale aliposema "Ni bora kufa kwa fikra ambayo itaishi kuliko kuishi kwa fikra ambayo itakufa".
Maana yake kwamba ni bora kufa(kufeli) kwa kupigania haki yako na kupata unachodai na pengine kikaendelea kusaidia kwa vizazi vijavyo kuliko kuogopa kupigania uhuru na haki yako ili hali wakati huo utapita na utaendelea kunyimwa haki(fasiri yangu).

Ndiyo, ni kweli wanafunzi hao waliamua kupigania haki yao hata kama wanaona itawasababisha wengine kufeli na kurudia mitihani,ama kurudia mwaka, ama kufeli zaidi na kurudi nyumbani lakini hata kama watafeli na kurudi nyumbani basi haki iliyopatikana itaendelea kusaidia kwa wale waliobaki na watakaokuja.

Hii naifanisha tu na wapigania uhuru wengine wa kiafrika kama akina Patrice Lumumba, Stephen Biko, Nyerere, Nkruma, wao naamini hawakuangalia pande hasi bali ni pande chanya kwao, yaani kitakachopatikana kitaendelea kusaidia vizazi vijavyo kama sisi tunavyofaidi matunda ya uhuru.

Pengine suala kubwa la kujiuliza kwa nini kumekuwepo na mapinduzi na migomo ya mara kwa mara vyuoni nchini na pengine kwa Mzumbe(hasa katika serikali ya wanafunzi)?.

Kuna haja ya kuliangalia hasa kwa pande zote mbili.Mosi ni kwa upande wa wanafunzi wenyewe.Pili ni kwa upande wa Uongozi wa juu wa chuo(Menejimenti).

Kwa vyovyote na uhakika pande hizi mbili zinahusika moja kwa moja katika migogoro mingi katika vyuo vyetu na taasisi za elimu za juu hapa nchini.

Mfano mjini mzumbe Uongozi uliokuwepo wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo kwa maana ya MUSO, chini ya rais wake bwn INNOCENT LAZARO MGETA, ilidaiwa ni mbovu na ilishindwa kutekeleza matakwa ya wananchi wake na hatimae ikawa inajali maslahi binafsi kama wabunge wetu walipoamka na madai ya maslahi manene kabla ya maslahi ya umma.

Mapinduzi yalifanyika na bwn PIUS KAHESHI anayesoma shahada ya kwanza ya utawala wa biashara katika manunuzi na ugavi na aliyekuwa nje ya chuo kwenye mafuzo kwa vitendo(FIELD) ndo aliibuka kidedea kwa kupendekezwa na wananchi mpaka kuitwa kwa haraka kutoka Dar es salaam ili aende kuogoza umma wa wanamzumbe.

Hii kwangu binafsi ilinipa maswali mengi na kupata jibu moja toshelevu kwamba ni kweli uongozi huo ulikuwa haufai na wananchi waliuochoka.
Iweje leo wananchi waamue kuiondoa serikali na mtu wa kushika akatoka mbali na nje ya chuo ingawa ni mwanafunzi lakini gharama ya kumwita na ndani ya masaa angalau 2 anakuwa ameshafika?.
Basi tukubali kwamba huyu Bwn PIUS KAHESHI ni kiongozi bora kama viongozi wowote duniani kwa mtazamo wa uongozi katika jamii husika.Kwani hapakuwepo na watu mbadala wa kuwekwa baada ya vuguvugu la mapinduzi mpaka akaitwa huyu Kaheshi toka DSM KARIBU UMBALI WA kilomita 122 toka dsm mpaka mzumbe?.

Basi tukubali kwamba huyu bwn Mgeta hafai pamoja na kuwa mtaalamu wa sheria ambae wananchi walitegemea aongoze kwa utawala bora na wa sheria kwa vile ni mtalaamu wa sheria.

Pengine tukubali kwamba alikuwa anakumbatiwa na menejimenti ya chuo kwa vile mpaka sasa menejiment hiyo imeshindwa kukubaliana na matakwa ya wananchi ya kumuondoa Mgeta na imechukua mda wa wiki moja na sasa inadaiwa hakuna serikali ya MUSO.

Pengine tukubali kwamba viongozi kama akina Mgeta ndo wale wale wanaokuja kuwa viongozi si wenye kujali maslahi ya umma hata baada ya kutoka mzumbe kwa vile ameshindwa kutekeleza matakwa na kuleta maslahi ya wanafunzi ndani ya miezi takribani saba tu tangu aingie madarakani.

Nasema hivi kwa sababu nategemea viongozi walio wengi wa kitaifa na kimataifa huanzia sehemu kama hizi kwa vipimo vyao vya uongozi bora.
Nilipata kumsoma mwandishi mmoja katika makala moja kwenye gazeti la kiswahili hapa nchini kwamba rais Jakaya Kikwete alikuwa na wazo la kuwa atakuja kuwa rais wa nchi hii mwaka 1975, kwa maana kwamba nyakati hizo alikuwa ama shuleni au chuoni na akiwa kiongozi.Hilo mimi nilisoma tu kama unataka uhakika muulizeni mheshimiwa rais.

Kwa upande mwingine.Nilisema kwamba migogoro chuoni ama mashuleni yaweza kusababishwa na uongozi mbovu wa utawala wa chuo, kwani inapofika pahala maslahi ya wanafunzi hayatekelezwi ipasavyo na kuonekana ni kama watu wasio elewa haki zao basi hapo solution ya wanafunzi huwa ni kugoma au kuleta fujo.

Hata hivyo ni fikra finyu na potofu kwa jamii yetu na serikali kwa ujumla kuwa wanakariri kwamba migogoro kama migomo ya wanafuzi ni ukorofi wa wanafunzi wenyewe, bila ya kuangalia na upande wa uongozi wa juu wa chuo.

Madai ya wanafunzi huwa ni sawa na madai ya mtu yeyote anayepigania haki yake.na kama sivyo, basi kuwepo na commission maalumu ya kuwa inafuatilia migogoro hiyo na kutoa taarifa kwa mheshimiwa rais au wizara husika.

Labda tu niseme na kumkumbusha mheshimiwa rais katika eneo hili kwani ni muhimu sana kwa maendeleo ya elimu yetu ya juu.
Mimi nashauri kwa rais kwamba ili kuleta tija ndani, na kuboresha utawala na uongozi bora vyuoni na hatimae kupunguza migogoro ya wanafunzi basi hakuna budi vile vile kuwepo na uwezekano wa kuwa, wakuu, (makamu wakuu wa chuo ambao ni watendaji wa shughuli zote chuoni) wasikae na kufanya kazi sehemu moja(chuo kimoja) si zaidi ya miaka 5 au miaka fulani. Sio kama ilivyo sasa unakuta mkuu wa chuo(Makamu mkuu) wa chuo anakaa sehemu moja zaidi ya miaka 10 au 25.
Hii kwangu naiona kama watu wengine(wakuu hao) hujisahau nakuzoea na kukifanya chuo kama taasisi binafsi ya kwake na vyovyote asemayo basi yeye ndiye yeye, wengine wasiamue, hakika huo sio utawala bora na hapo migogoro ndo inapoanzia.

Kwangu binafsi nilitegemea chuo kikuu kama cha Mzumbe kusiwe na migogoro ya migomo au mapinduzi ya aina yeyote kwani wao ndo kitovu cha fani za utawala na uongozi kama kilivyoanzishwa kama azima yake.
Hata Hayati Mwalimu Nyerere ni shahidi(Mungu aendelee kumuweka mahali pena peponi,Amina).Leo inakuja mgogoro kama wa wanafunzi unashindikana kutatuliwa kwa njia ya diplomasi na kutumia utawala wao na kubaki na majibu ya ama hakuna utambuzi wa serikali ya MUSO kwa pande wa uongozi uliokuwepo ama uliowekwa na wananchi walivyoamua kwa sasa.

Tuamini kwamba hata uongozi wa juu wa chuo haujui kutatua matatizo kama hayo kwa maslahi ya wengi?(Wanafunzi) mpaka wanaondoka wanafunzi kwenda likizo wakiwa wanaamini ama rais ni PIUS KAHESHI, na wengine wakiamini rais ni INNOCENT MGETA sanjali na kufungwa kwa ofisi ya serikali ya MUSO.

Je nani aliwaambia menejiment ya chuo kwamba wakati wa likizo hakuna matatizo ya wanafunzi na yanatakiwa kutatuliwa kwa njia au kupitia serikali yao?, sasa hawa wananchi hawana serikali inayotambulika, eti mpaka kufanyike ukaguzi wa matumizi ya fedha zilizotumika katika serikali iliyoondolewa madarakani na wananchi na uamuzi wa mwanasheria wa sehemu isiyofungamana na upande wowote, ili watoe ni nani anastahili kuwa rais wa MUSO.

Suala hili ni jambo jema na la haki.Lakini tujiulize wote mpaka inafikia hatua hiyo,je tuamini kwamba menejiment ya chuo ilishindwa kulitatua suala hilo mapema ? au ndo imetumia umahiri wa fani za mzumbe za utawala na uongozi kwa kuliweka suala hili katika hali tete kwamba mpaka uamuzi wa kisheria kutoka sehemu isiyofungamana na upande wowote?.Yangu macho, lakini nawatahadhalisha kwamba fanyeni haraka kabla ya likizo haijaisha na wenye serikali hawajarudi toka likizo mbona patakuwa padogo.
Hata hivyo umefika wakati kwa wanajamii wa vyuo vikuu kuacha ushabiki wa kikanda, kikabila, kidini, na kikozi kuchagua viongozi wabovu kwa kuzingatia kada za aina hiyo kwani zinazaa matunda tofauti na jamii ilivyotarajia.

Nyinyi ndo wanazuo na jamii ndo inatakiwa ijifunze kwenu katika chaguzi zenu na mchanganuo wenu wa fikra akinifu katika uchaguzi wa viongozi wa vyuoni mpaka wa kitaifa, la sivyo itakuwa hakuna maana ya kuwepo na wanazuo kama ninyi, kwa sababu hakuna jamii inalojifunza kutoka kwenu.

Isitoshe, kuna haja vile vile kwa upande wa serikali hasa kwa wizara husika kuaamka sasa na kuanza kusimamia na kufuatilia kwa chaki na rula maslahi na migogoro inayojitokeza vyuoni, ili kulinda heshima ya wasomi wetu ambao sasa wanaonekana kama wahuni wetu wanapoanza vuguvugu la madai chanya ya wanafunzi.Msiegemee upande mmoja tu kwamba wanafunzi wa vyuoni ni wakorofi, mtakuwa mnajenga chuki na gap kati ya wasomi na jamii, wasomi na serikali, na wasomi na uongozi wa vyuoni.
Hapo nafikiri mantiki ya kuwepo wasomi haitakuwa na maana.

"Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Mzumbe iweze kutatua mgogoro wa MUSO".

Wednesday, February 01, 2006

Kasi ya Ujambazi: Kinga ni bora kuliko tiba.

Mrema aulizwe alifanikiwaje kwa hili?

Kumekuwa na gumzo kutoka kila pembe ya nchi hii iitwayo ya amani na utulivu juu ya kuzidi kwa wimbi la ujambazi karibia nchi nzima.

Majambazi na ujambazi kwa vyovyote na kwa hali yeyote ile huleta athari ambazo ni kunyume na neno la Amani na utulivu katika jamii yeyote ile. Na kwamba ujambazi wa kuvamia sehemu mbalimbali nchini umepamba moto na badom unaendelea kutishia amani ya wananchi aidha wawapo kwenye kumbin za starehe, majumbani wamejipumzisha baada ya kazi zao za siku za kihalali, sokoni, madukani wakifanya shopping zao kama kariakoo na kwingineko. Kupamba moto huku kwa majambazi kulikuja tu baada ya serikali ya awamu ya nne kutangazwa na kuundwa wizara mahususi ya kupambana na uhalifu nchini, wizara ya Usalama wa raia chini ya waziri Kharith Bakari Mwapachu.

Hata hivyo, yamesemwa mengi na wanacnhi juu na kuhusu kilio, mapendekezo juu ya kukithiri kwa ujambazi au uhalifu wa majambazi nchini.
Kwangu binafsi sihitaji kuyarudia yoote yale ambayo yameshasemwa na waliotangulia wananchi wenzangu kwa serikali, lakini labda nizidi tu kuongezea pale paliposahaulika au kama wazo mbadala kwa serikali ya wana ari, nguvu na Kasi mpya juu ya kulidhibiti janga hili la ujambazi kwa watanzania wasio na hatia na wanaojitafutia ridhiki zao kiuhalali.

Napenda na kwa mapenzi yote ya nchi yangu na watu wake, naishauri serikali ya awamu ya nne chini ya wizara ya usalama wa raia kwamba kama ujambazi na majambazi yanashindikana kudhibitiwa na vitendo vyao, Basi serikali haina budi na isione aibu yeyote kumuuliza Mheshimiwa(kwangu) Agustino L.Mrema, Mwenyekiti wa chama cha TLP, ni kwa jinsi gani?, njia zipi? Na kwa vipi yeye binafsi alikuwa akizitumia na kuweza kudhibiti na kupunguza wimbi la ujambazi na athari zake twaweza kusema ni kwa zaidi ya asilimia 80 alipokuwa waziri wa mambo ya ndani?.

Hili kwa mtanzania yeyote ni shahidi kwa serikali ya awamu ya pili Mrema alipoagiza majambazi sugu na silaha zao kuzisalimisha kituo cha polisi chochote nchini kabla ya wao hawajatiwa mikononi mwa serikali. Wala hatujasahu hilo na hakuna asiyefahamu na kwa hilo Mrema nampongeza. Kwa mantiki hiyo juhudi za Mrema kwa jambo hili waweza kuzilinganishaje na juhudi za sasa katika ujambazi pamoja na kuwepo wizara maalum ya kushughulikia suala kama hili?, au ndo imekuwa kama wametria petroli kwenye moto unaowaka kuuongezea?. Hali inazidi kutisha, wananchi wanauawa, mali zao zinapokonywa na kurudishwa kwenye umaskini huu huu tunaoupigania kuuondoa kwa kutumia MKUKUTA unakuwa kikwazo kwa Ujambazi.

Isitoshe, kama mheshimiwa rais aliposema baada ya kuapishwa uwanja wa taifa, aliwaambia wana-CCM kuwa wasiwabeze sana wapinzani kwani hata wao wapo waliowapa kura na sasa hatuna budi kuacha kugombana na kuanza kuzima moto unaoteketeza nyumba yetu. Na hivyo ndivyo hivyo, mamuomba Mheshimiwa Mrema kwa kuzingatia busara zake na busara ya Mheshimiwa rasi aliyoisema basi atakapoitwa asisite kuwasaidi watanzai mikakati aliyoitumia kudhibiti ujambazi.

Na wewe mheshimiwa Mwapachu nakuomba kwa niaba ya wananchi wenzagu acha kuficha maradhi, kifo kitakuumbua, anika matatizo yako ya ujambazi kwa A.L.Mrema upate fimbo na dawa kwa wizara yako inayoonekana ni ngumu, na kweli ngumu kwa hali inavyotisha sasa.Bwana Mrema kwa imani yangu anatupenda wanachi wake na ana uchungu na nchi yake, na ndo maana huwa yupo kutetea kwa lolote kama serikali haitendi yaliyo haki na kwa mantiki hiyo tunaomba kwa pande zote make mjadiliane.Jamni si tunajenga nyumba moja, basimtusaidiane huyu kuleta bati, huyu ufito, huyu mfuko wa simentio ili mradi nyumba bora ikamilike,Mrema saidia , Mwapachu kaa na huyu mheshimiwa muulize atakusaidia tuu.

Nafikiri hapatakuwa na aibu yeyote kwa serikali yetu kupata njia mbadala kutoka kwa watu mbalimbali na si kauli za kuua muwapatapo majambazi.je chanzo chake mnacho?,dalili zake je?, mmh! Yangu macho.

"Kwa ukweli huu sitakuwa adui kwa serikali yangu ."