Saturday, February 04, 2006

CHUO KIKUU KIKUU MZUMBE NA HATIMA YA MAPINDUZI YA SERIKALI(MUSO).

Ni pale tu uongozi uliopo madarakani unaposhindwa kukidhi na kutekeleza yale iliyoahidi kwa wananchi wake, ndipo wanachi wale wale hurudi na kutaka kuiondoa serikali husika kwa vile imekwenda kinyume na ilichokiahidi kwa hadhira husika.

Ilikuwa ni jumamosi ya tarehe 28, january 2006, ndipo mgogoro wa mapinduzi ya serikali ya wanafunzi Mzumbe ulipoanza na kujitokeza masikioni mwa wakazi wa wananchi wa Mzumbe chuoni pamoja na majirani zake na kesho yake taarifa zikawa zimeenea karibu nchi nzima.Mgogoro huo umeendelea mpaka siku ya wiki iliyofuata ya tarehe 3, February 2006, na kwa maana nyingine mgogoro wa kuipindua serikali iliyokuwa madarakani imechukua mda wa wiki nzima.

Hata hivyo mapinduzi hayo yalifanyika na yaliendelea kufanyika ili hali wanafunzi wakiwa wanaendelea na mitihani yao ya semista ya kwanza.Hawakuchelea pamoja na kuwa walikuwa na mzigo wa mitihani hiyo, lakini waliona bora kujikomboa kutoka uongozi mbovu uliokuwepo wa MUSO na pengine hata menejiment ya chuo.

Nasema hivi kwa sababu kuna haja gani kwa wananchi wa mzumbe kutaka kuiondoa serikali husika ndani ya mitihani ama ingelikuwa nchi kamili ni katikati ya kukuza uchumi na kwenye matatizo kama ya njaa kwani mitihani ni kama kupanda na hatimae ukavuna.
Lakini hapo waweza kuvuna au kukosa na ndo hapo hufanana na kufeli kwa maana ya mazingira ya wanachuo.Lakini hayo yoote hawakuangalia wanajumuia wa Mzumbe, wakaamua kumwondoa labda nduli wao, ili wajikomboe.

Wananchi wa Mzumbe niliwafananisha na Bwn Stephen Biko wa Afrika Kusini pale, mpigania uhuru wa afrika kusini pamoja na akina Mandela pale aliposema "Ni bora kufa kwa fikra ambayo itaishi kuliko kuishi kwa fikra ambayo itakufa".
Maana yake kwamba ni bora kufa(kufeli) kwa kupigania haki yako na kupata unachodai na pengine kikaendelea kusaidia kwa vizazi vijavyo kuliko kuogopa kupigania uhuru na haki yako ili hali wakati huo utapita na utaendelea kunyimwa haki(fasiri yangu).

Ndiyo, ni kweli wanafunzi hao waliamua kupigania haki yao hata kama wanaona itawasababisha wengine kufeli na kurudia mitihani,ama kurudia mwaka, ama kufeli zaidi na kurudi nyumbani lakini hata kama watafeli na kurudi nyumbani basi haki iliyopatikana itaendelea kusaidia kwa wale waliobaki na watakaokuja.

Hii naifanisha tu na wapigania uhuru wengine wa kiafrika kama akina Patrice Lumumba, Stephen Biko, Nyerere, Nkruma, wao naamini hawakuangalia pande hasi bali ni pande chanya kwao, yaani kitakachopatikana kitaendelea kusaidia vizazi vijavyo kama sisi tunavyofaidi matunda ya uhuru.

Pengine suala kubwa la kujiuliza kwa nini kumekuwepo na mapinduzi na migomo ya mara kwa mara vyuoni nchini na pengine kwa Mzumbe(hasa katika serikali ya wanafunzi)?.

Kuna haja ya kuliangalia hasa kwa pande zote mbili.Mosi ni kwa upande wa wanafunzi wenyewe.Pili ni kwa upande wa Uongozi wa juu wa chuo(Menejimenti).

Kwa vyovyote na uhakika pande hizi mbili zinahusika moja kwa moja katika migogoro mingi katika vyuo vyetu na taasisi za elimu za juu hapa nchini.

Mfano mjini mzumbe Uongozi uliokuwepo wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo kwa maana ya MUSO, chini ya rais wake bwn INNOCENT LAZARO MGETA, ilidaiwa ni mbovu na ilishindwa kutekeleza matakwa ya wananchi wake na hatimae ikawa inajali maslahi binafsi kama wabunge wetu walipoamka na madai ya maslahi manene kabla ya maslahi ya umma.

Mapinduzi yalifanyika na bwn PIUS KAHESHI anayesoma shahada ya kwanza ya utawala wa biashara katika manunuzi na ugavi na aliyekuwa nje ya chuo kwenye mafuzo kwa vitendo(FIELD) ndo aliibuka kidedea kwa kupendekezwa na wananchi mpaka kuitwa kwa haraka kutoka Dar es salaam ili aende kuogoza umma wa wanamzumbe.

Hii kwangu binafsi ilinipa maswali mengi na kupata jibu moja toshelevu kwamba ni kweli uongozi huo ulikuwa haufai na wananchi waliuochoka.
Iweje leo wananchi waamue kuiondoa serikali na mtu wa kushika akatoka mbali na nje ya chuo ingawa ni mwanafunzi lakini gharama ya kumwita na ndani ya masaa angalau 2 anakuwa ameshafika?.
Basi tukubali kwamba huyu Bwn PIUS KAHESHI ni kiongozi bora kama viongozi wowote duniani kwa mtazamo wa uongozi katika jamii husika.Kwani hapakuwepo na watu mbadala wa kuwekwa baada ya vuguvugu la mapinduzi mpaka akaitwa huyu Kaheshi toka DSM KARIBU UMBALI WA kilomita 122 toka dsm mpaka mzumbe?.

Basi tukubali kwamba huyu bwn Mgeta hafai pamoja na kuwa mtaalamu wa sheria ambae wananchi walitegemea aongoze kwa utawala bora na wa sheria kwa vile ni mtalaamu wa sheria.

Pengine tukubali kwamba alikuwa anakumbatiwa na menejimenti ya chuo kwa vile mpaka sasa menejiment hiyo imeshindwa kukubaliana na matakwa ya wananchi ya kumuondoa Mgeta na imechukua mda wa wiki moja na sasa inadaiwa hakuna serikali ya MUSO.

Pengine tukubali kwamba viongozi kama akina Mgeta ndo wale wale wanaokuja kuwa viongozi si wenye kujali maslahi ya umma hata baada ya kutoka mzumbe kwa vile ameshindwa kutekeleza matakwa na kuleta maslahi ya wanafunzi ndani ya miezi takribani saba tu tangu aingie madarakani.

Nasema hivi kwa sababu nategemea viongozi walio wengi wa kitaifa na kimataifa huanzia sehemu kama hizi kwa vipimo vyao vya uongozi bora.
Nilipata kumsoma mwandishi mmoja katika makala moja kwenye gazeti la kiswahili hapa nchini kwamba rais Jakaya Kikwete alikuwa na wazo la kuwa atakuja kuwa rais wa nchi hii mwaka 1975, kwa maana kwamba nyakati hizo alikuwa ama shuleni au chuoni na akiwa kiongozi.Hilo mimi nilisoma tu kama unataka uhakika muulizeni mheshimiwa rais.

Kwa upande mwingine.Nilisema kwamba migogoro chuoni ama mashuleni yaweza kusababishwa na uongozi mbovu wa utawala wa chuo, kwani inapofika pahala maslahi ya wanafunzi hayatekelezwi ipasavyo na kuonekana ni kama watu wasio elewa haki zao basi hapo solution ya wanafunzi huwa ni kugoma au kuleta fujo.

Hata hivyo ni fikra finyu na potofu kwa jamii yetu na serikali kwa ujumla kuwa wanakariri kwamba migogoro kama migomo ya wanafuzi ni ukorofi wa wanafunzi wenyewe, bila ya kuangalia na upande wa uongozi wa juu wa chuo.

Madai ya wanafunzi huwa ni sawa na madai ya mtu yeyote anayepigania haki yake.na kama sivyo, basi kuwepo na commission maalumu ya kuwa inafuatilia migogoro hiyo na kutoa taarifa kwa mheshimiwa rais au wizara husika.

Labda tu niseme na kumkumbusha mheshimiwa rais katika eneo hili kwani ni muhimu sana kwa maendeleo ya elimu yetu ya juu.
Mimi nashauri kwa rais kwamba ili kuleta tija ndani, na kuboresha utawala na uongozi bora vyuoni na hatimae kupunguza migogoro ya wanafunzi basi hakuna budi vile vile kuwepo na uwezekano wa kuwa, wakuu, (makamu wakuu wa chuo ambao ni watendaji wa shughuli zote chuoni) wasikae na kufanya kazi sehemu moja(chuo kimoja) si zaidi ya miaka 5 au miaka fulani. Sio kama ilivyo sasa unakuta mkuu wa chuo(Makamu mkuu) wa chuo anakaa sehemu moja zaidi ya miaka 10 au 25.
Hii kwangu naiona kama watu wengine(wakuu hao) hujisahau nakuzoea na kukifanya chuo kama taasisi binafsi ya kwake na vyovyote asemayo basi yeye ndiye yeye, wengine wasiamue, hakika huo sio utawala bora na hapo migogoro ndo inapoanzia.

Kwangu binafsi nilitegemea chuo kikuu kama cha Mzumbe kusiwe na migogoro ya migomo au mapinduzi ya aina yeyote kwani wao ndo kitovu cha fani za utawala na uongozi kama kilivyoanzishwa kama azima yake.
Hata Hayati Mwalimu Nyerere ni shahidi(Mungu aendelee kumuweka mahali pena peponi,Amina).Leo inakuja mgogoro kama wa wanafunzi unashindikana kutatuliwa kwa njia ya diplomasi na kutumia utawala wao na kubaki na majibu ya ama hakuna utambuzi wa serikali ya MUSO kwa pande wa uongozi uliokuwepo ama uliowekwa na wananchi walivyoamua kwa sasa.

Tuamini kwamba hata uongozi wa juu wa chuo haujui kutatua matatizo kama hayo kwa maslahi ya wengi?(Wanafunzi) mpaka wanaondoka wanafunzi kwenda likizo wakiwa wanaamini ama rais ni PIUS KAHESHI, na wengine wakiamini rais ni INNOCENT MGETA sanjali na kufungwa kwa ofisi ya serikali ya MUSO.

Je nani aliwaambia menejiment ya chuo kwamba wakati wa likizo hakuna matatizo ya wanafunzi na yanatakiwa kutatuliwa kwa njia au kupitia serikali yao?, sasa hawa wananchi hawana serikali inayotambulika, eti mpaka kufanyike ukaguzi wa matumizi ya fedha zilizotumika katika serikali iliyoondolewa madarakani na wananchi na uamuzi wa mwanasheria wa sehemu isiyofungamana na upande wowote, ili watoe ni nani anastahili kuwa rais wa MUSO.

Suala hili ni jambo jema na la haki.Lakini tujiulize wote mpaka inafikia hatua hiyo,je tuamini kwamba menejiment ya chuo ilishindwa kulitatua suala hilo mapema ? au ndo imetumia umahiri wa fani za mzumbe za utawala na uongozi kwa kuliweka suala hili katika hali tete kwamba mpaka uamuzi wa kisheria kutoka sehemu isiyofungamana na upande wowote?.Yangu macho, lakini nawatahadhalisha kwamba fanyeni haraka kabla ya likizo haijaisha na wenye serikali hawajarudi toka likizo mbona patakuwa padogo.
Hata hivyo umefika wakati kwa wanajamii wa vyuo vikuu kuacha ushabiki wa kikanda, kikabila, kidini, na kikozi kuchagua viongozi wabovu kwa kuzingatia kada za aina hiyo kwani zinazaa matunda tofauti na jamii ilivyotarajia.

Nyinyi ndo wanazuo na jamii ndo inatakiwa ijifunze kwenu katika chaguzi zenu na mchanganuo wenu wa fikra akinifu katika uchaguzi wa viongozi wa vyuoni mpaka wa kitaifa, la sivyo itakuwa hakuna maana ya kuwepo na wanazuo kama ninyi, kwa sababu hakuna jamii inalojifunza kutoka kwenu.

Isitoshe, kuna haja vile vile kwa upande wa serikali hasa kwa wizara husika kuaamka sasa na kuanza kusimamia na kufuatilia kwa chaki na rula maslahi na migogoro inayojitokeza vyuoni, ili kulinda heshima ya wasomi wetu ambao sasa wanaonekana kama wahuni wetu wanapoanza vuguvugu la madai chanya ya wanafunzi.Msiegemee upande mmoja tu kwamba wanafunzi wa vyuoni ni wakorofi, mtakuwa mnajenga chuki na gap kati ya wasomi na jamii, wasomi na serikali, na wasomi na uongozi wa vyuoni.
Hapo nafikiri mantiki ya kuwepo wasomi haitakuwa na maana.

"Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Mzumbe iweze kutatua mgogoro wa MUSO".

3 Comments:

At 10:06 AM, Blogger boniphace said...

Nimekusoma sana nini hasa sababu ya kumfuata huyo jamaa huko Dar au huko ndiko alikokuwa akiandalia Mapibnduzi. Nieleze pia nini sababu za wakazin kuchoka serikali yao ambazo zinashikika.

 
At 2:44 AM, Blogger JUNGU KUU, Kwa fikra akinifu said...

Bwana Makene, huyu Bwn PIUS KAHESHI alifuatwa huko DSM akiwa field(Practical Training) ambapo kwa utaratibu wa chuo kikuu mzumbe huchukua semester yoote kuanzia october ya kila mwanzo wa mwaka mpaka mwishoni mwa january ya kila mwaka kwa kila mwaka wa mwisho wa masomo.kwa hiyo ni wananchi walioamua kuing'oa serikali yao walioiweka wao wenyewe.
Na huyu bwn Pius alikuwa mmoja wa wagombea na akishindwa na akawa mshindi wa pili,.Lakini ndo hivyo ilionekana huyu bwn Mgeta alishinda kwa makundi ya kufuta ukozi kama nilivyoeleza.
Baada ya kushindwa bwn mgeta kufuatilia bum na madai mengine ya kishule mzumbe basi wananchi wakaamua kumwondoa madarakani.
Nafikiri umenipata mpaka hapo.

 
At 2:46 AM, Blogger JUNGU KUU, Kwa fikra akinifu said...

ANGALIA COMMENTS

 

Post a Comment

<< Home