Friday, February 17, 2006

MRADI WA MAJI ZIWA VICTORIA ULENGE 2050;
Ni katika kukabiliana na ukame mkali ujao
Mradi uweze kutumika kuzalisha chakula cha kutosha.


Ilikuwa ni faraja na neema kwa wakazi wote wa mikoa ya kanda ya ziwa, hasa mkoa wa shinyanga kwa kupitishwa mkakati na mradi mkubwa wa maji wa ziwa victoria, miaka kama miwili hivi iliyopita.Na nina imani mradi huo kwa sasa unaendelea chini ya wachina waliopewa ukandarasi wa kujenga.Hata hivyo si mkoa wa shinyanga pekee uliolengwa katika mradi huo, hii ilikuwa ni pamoja na mikoa ya Mwanza, Tabora na hatimae utafika mpaka makao makuu ya nchi Dodoma hata kama kwa miaka kumi na tano ijayo.

Pengine tutakumbuka, mheshimiwa waziri mkuu wa sasa, Edward Ngoyai Lowasa ndiye aliyesimama kidete bila kuteteleka na kurudi nyuma katika kuutetea mradi huu uendelee kujengwa baada ya Misri kuleta kikwazo kwamba ni wao pekee ndio wenye mamlaka ya kutumia maji ya ziwa victoria kutokana na mkataba wa kikoloni uliowaruhusu kufanya hivyo na si nchi nyingine yeyote.
Lakini hilo Lowasa hakuangalia makunyanzi ya wana wa farao, yeye akawa kama jiwe la pembeni lililowashinda waashi, basi lingewaangukia na kuwaponda na kuwasaga, huoo, mradi uliendelea mpaka sasa.
Nami nachukua fursa hii kumpongeza mheshimiwa waziri mkuu kwa kuwa shujaa kwa kiasi hicho kwa maslahi ya nchi yake.

Inatosha tu, kusema kwamba mradi huu wa maji kutoka ziwa victoria ili unufaishe wananchi woote katika sehemu ulikoanzia , kupitia mpaka utakapoishia kwa awamu, kama sikosei itakuwa awamu ya kwanza ililengwa utaishia wilaya ya Kahama mkoani shinyanga.
Mradi huu naomba ulenge hasa katika kuwezesha kilimo cha tija zaidi kwa sehemu itayonufaika na mradi huu.Mradi wa maji haya usilenge tu kama maji ya matumizi ya kawaida ya wakazi husika, kwani ni mradi ambao umetumia pesa nyingi mno za kwetu ndani na toka kwa wafadhiri nje.

Kama vile haitoshi, mradi huu ulenge ukame mkali sana ambao unasemekana utabisha hodi ifikapo 2050, pengine hata kabla ya huko kama tunavyojionea wenyewe sasa hivi.Mradi huu ukilenga mbali zaidi utatuwezesha kukuta tuna vyakula vya kutosha kwenye maghala yetu ya chakula ya kila kanda kama yapo, au maghala mahususi kwa kuhifadhi mazao mbalimbali.

Ninaonavyo mimi, hata kama shinyanga na mikoa hiyo ya kanda ya ziwa watazalisha dengu pekee, basi wazalishe dengu nyingi na za kutosha kwa kutumia mradi huu wa maji kwa kufanya kilimo cha umwagiliaji ili waweze kulisha watanzania wote ifikapo miaka hiyo ya ukame mkali 2050 kama inavyosemekana.

Nasema hivi kwa sababu, nimekutana na tafakuri ya Profesa Charles Bwenge, Mhadhiri wa Lugha katika chuo kimojawapo huko Marekani. Tafakuri yake ililenga katika upungufu wa chakula nchini.Tafakuri yake aliitoa katika gazeti mojawapo la kiswahili litolewalo mara moja kwa wiki, la tarehe 16-22, Februari 2006 katika ukurasa wa 12.

Profesa Charles Bwenge anasema "Kikundi cha watafiti nchini Uingereza kinachochunguza kuongezeka kwa joto duniani miaka minane iliyopita kilitabiri kuwa maeneo mengi barani Afrika yatakumbwa na ukame mkali sana ifikapo 2050, na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula utakaoathiri watu zaidi ya millioni thelathini(30).".Mwisho wa kumnukuu.
Binafsi mawazo ya Prof.Bwenge yaliniingia na kufikiri kwamba mwenye macho haambiwi tazama, tayari sasa joto hilo la ukame tumeanza kulionja, kwa nini tusubiri mpaka 2050?, basi napenda kuwakumbusha watanzania kutokana na hoja ya Prof. Bwenge kwamba tujiandae ipasavyo hasa kwa kuutumia mradi huu mkubwa toka ziwa victoria kama nionavyo mimi.Na tena si hivyo tu kuwepo na mpango maalumu wa kuanzisha mazao yapi yaanze na yanastahili kwa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika maeneo ya sehemu itakakopita mradi huu.

Prof.Bwenge, hata hivyo anaongeza kwa kusema kwamba, namnukuu," Ni dhahiri kuwa upungufu wa chakula ni matokeo ya mipango mibovu ya serikali katika miaka kumi, au ishirini au zaidi iliyopita, na kama hakuna hatua madhubuit zinazochukuliwa kuboresha sekta ya kilimo na techonolojia ya kuhifadhi chakula kinachozalishwa, basi huo mwaka 2050, tutakipata.Tusije kulaumu ukame"

Binafsi naungana na Prof.huyu kwa asilimia mia moja, kwani mawazo na fikra hizo zimetolewa katika muda muafaka kabisa kwa hiyo hatuna budi kujiandaa kuelekea 2050 hata kabla ya hapo, kama ilivyo sasa.
Ni muda muafaka vile vile kuanzishwa kwa mradi huu wa ziwa victoria kwani utasaidia sana katika maendeleo ya kilimo ksichotegemea msimu wa mvua sanjari na jitihada za watalaamu wa wetu wa kilimo kubaini ni mazao yapi yanastahili yapewa kipaumbele katika sehemu unakopita mradi huu, ili wananchi wa sehemu hizo wazalishe mazao hayo kwa ubora zaidi na kwa wingi zaidi kulenga 2050, kwenye ukame mkali.
Hata hivyo, niliwahi kuandika makala yangu gazeti la Mtanzania kwamba ni wakati sasa mzuri kwa watalaamu wetu wa kilimo kurudi katika fani yao ya kilimo na kwa wakulima na si kukaa maofisini tu na kutaka kufanya kazi zingine tofauti na walizosomea.
Lengo la makala hiyo ni kuwakumbusha watalaamu hawa kukiboresha kilimo chetu kilcho hoi bin taabani, ili hali tukisema kwamba eti kilimo Tanzania ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Hii ni kudanganyana, kwani tangu lini ukakuta uchumi wa nchi unategemea asilimia zaidi ya themanini(80) ya wakazi wake ni wakulima wadogo wadogo(Peasants)?, tena wakitumia jembe la mkono ukasema uchumi unatokana na kilimo cha aina hiyo?.

Kwa mantiki hii kwa nini tusisote kwa kukumbwa na ukame na jaa ya kishindo kwa vile kilimo chetu ni cha Pure subsitence farming system(Peasants), ambao wanatumia jembe la mkono katika kati ya bwawa la utandawazi na technolojia lukuki za kilimo, na mingineyo?.Au hapa hatujaligundua hili kwamba Tanzania bado tunacheza makida makida kwenye suala zima la kilimo.

Labda naomba ni jibiwe swali hili, ni asilimia ngapi Tanzania ni wakulima kwa maana ya mkulima(Farmers) na si wakulima wadogowadogo(Peasants)?,Kama wapo asilimia fulani ni kiasi gani huzalisha kutoka kwenye kilimo, na kwa nini tunasota kwa njaa sasa?.
Hapa nina uhakika hakuna jibu la moja kwa moja lakini jibu litaanzia na Inategemea.Pengine nsivuke kwenye mada yangu, ila tu nazidi kuungana mkono na Prof.Charles kwamba upungufu wa chakula nchini ni kwa sababu ya mipango mibovu ya serikali katika miaka 10 au zaidi iliyopita, na hakuna budi sasa serikali kuling'amua hilo na lianze kufanyiwa kazi mara moja.

Kama hivyo ndivyo, natoa wito na waraka wangu huu vile vile kwa serikali ya awamu ya nne ya wana Kasi mpya na wana kiwango cha kasi ya kutosha na umahiri uliobobea kuanza kuweka mipango mizuri kabisa na ya makusudi katika kilimo cha umwagiliaji wa kutumia mradi wa ziwa victoria.Vinginevyo, mradi utakuwepo na maji yatakuwepo, ila ifikapo 2050, tutakumbwa na huo ukame mkali, na njaa, halafu tutamalumu nani?.Na fikiri lawama za kwanza zitakwenda kwa woote walio kwenye dhamana ya kupanga mipango mahususi ya kilimo bora na chenye tija.Tutawalaumu hata kama watakuwa wazee wasiojiweza na wenye kutembelea mikongojo, lawama hatazikwepa.
Nasema lawama hawazikwepa kwa vila walitakiwa kuyazingatia mawazo yetu ya sasa ya mipango ya mbele kabisa na kuyapa kipaumbele zaidi katika vikao vyao mbalimbali vya taifa kama bunge au semina kama za wabunge, na wasianze na maslahi binafsi, mmh, acha nisitoneshe kidonda.

Namalizia kwa kusema kwamba, mipangi mizuri na mafanikio mazuri hupatikana pale penye nia na njia ya mipango ya mda mrefu(Long term Plan), na si papo kwa hapo.Kwa wadau, wananchi, na serikali kwa ujumla angalau yasomeni mawazo haya na myaandike kwa kalamu ya risasi, japo yatakuwa yanaonekana kwenye karatasi mlipoandika, yaweza kuja kukumbukwa na kuhitajika ifikapo kwenye kilio cha kusaga meno hapo panapotabiriwa kwenye ukame mkali 2050.

Naomba tusije rudi nyuma na kukumbuka kwamba penye miti mingi hapana wajenzi wakati tutaungana kati ya watu milioni 30 wakiugumia kwa njaa na ukame wakati tuna mradi mkubwa wa ziwa victoria.

'Sawa, kasi mpya kwenu katika kilimo cha jembe la mkono", Tusije laumu ukame na njaa ifikapo 2050.

4 Comments:

At 3:57 AM, Blogger mwandani said...

Naam, namuafiki Bw. Bwenge kabisa kuwa upungufu wa chakula ni mipango mibovu, na hakuna sababu ya kupungukiwa chakula.
Kimaendeleo tumepishana lakini kama huku barani Australia - inasemekana Australia ndio bara kame kuliko yote, asilimia 60 ya bara hili hakukaliki, lakini pamoja na ukame wa kila mara chakula kinatosha wakati wote, mipango ya muda mrefu ya kukabili mabalaa (disaster risk preparedness and mitigation - hili ni somo katika shahada ya mwanamaendeleo yoyote, na viongozi pamoja na wataalamu wetu lazima walifaulu somo hili ili kuchukua shahada - hivyo wanaujua mchezo mzima)ndiyo inayotakiwa.

Kuhusu ziwa nyanza kutumika kwa ajili ya kilimo hilo ni jambo zuri pia,
lakini Uganda (Uganda Electricity Generating Company) imejenga kituo cha umeme kinyemela, hivi sasa maji ya ziwa hilo yanadidimia kwa kasi sana - asilimia 55 zaidi ya ilivyokuwa kabla ya bwawa la kituo cha umeme kujengwa.

tafadhali tembea kiungo hichi:

http://www.mg.co.za/articlepage.aspxarea=/breaking_news/breaking_news__africa/&articleid=263720

Jionee mwenyewe.

 
At 3:58 AM, Blogger mwandani said...

http://www.mg.co.za/articlepage.aspx?area=/breaking_news/breaking_news__africa/&articleid=263720

Hapo juu kiungo hakikukubali. Nimejaribu tena.

 
At 4:00 AM, Blogger mwandani said...

http://www.mg.co.za/articlepage.aspx?area=/breaking_news/
breaking_news__africa/
&articleid=263720

Unganisha kiungo hicho hapo juu kuwa neno moja, pengine utakutana na makala ninayoizungumzia.

 
At 9:21 AM, Blogger zarena kewat said...

That's what everyone likes. You have a good imagination. Great post thanks you
vimax canada

 

Post a Comment

<< Home