Tuesday, February 14, 2006

OPERATION ELIMU TABORA NI LAZIMA (OETL):Yahitajika.

Wakati mkoa wa Shinyanga umeweka operation okoa Shinyanga ni Lazima, basi wana Tabora nao hawana budi kuwa na operation Elimu Tabora ni Lazima(OETL).
Mkakati wa operation ya wana shinyanga inajumuisha pamoja na kuuokoa mkoa huu kiuchumi, kielimu, kiafya na mambo mengine yanayohitasjika kuinua shinyanga kimaendeleo na maisha ya wanashinyanga.

Hata hivyo, nimeona ni bora, nami niweze kuweka waraka huu kwa wanatabora, wadau na watu wote wenye mapenzi mema na mkoa huu wa kihistoria na wazamani nchini, ambao unazidi kudorora kila kukicha na siku hadi siku katika nyanja zote mpaka kwa maisha ya wananchi wa Tabora.
Sihitaji kutaja kila nyanja na matatizo yanayoukabili mkoa huu.Kwa matatizo kwa kweli yapo mengi, lakini kutokana na mada yangu nitajikita zaidi katika operation ya elimu mkoani humo.

Mimi kama mdau,na mzaliwa wa mkoa huu huwa napata shida na inakuwa hainingii akilini mwangu kila mwaka nikisikia, kuona elimu mkoani Tabora ikishuka, kwa maana kuna mfululizo wa miaka kadhaa imepita mpaka mwaka jana Tabora inakuwa inashika nafasi ya mwisho katika matokeo ya elimu ya msingi na ikipokezana na Shinyanga, ama shinyanga ya mwisho, ikifuatiwa na Tabora ya pili toka mwisho, ama Tabora ya mwisho na Shinyanga inafuatia, vivyo hivyo, mpaka aibu na inakera kwa wazalendo wa mkoa huu.

Nasema mpaka mwaka jana kwa maana ya matokeo ya mtihani wa mwaka jana yaliyotolewa mwaka huu kwa watahiniwa wa darasa saba.Bado Tabora ya mwisho, ingawa wenye dhamana ya kusimamia elimu mkoani humo walisema mwaka huu eti Tabora elimu imepanda kwa kushika nafasi ya kumi na kitu.

Mimi sikubaliani na takwimu hizo, kwani ningelikubaliana na kupanda kwa elimu kama Tabora ningesikia wameshika nafasi ya na wako katika kumi(10) bora, kwa vile imeabika siku nyingi mno kuwa ya mwisho, ndio hapo ningeliamini kweli kweli Tabora elimu imeboreshwa na kufaulisha vya kutosha.
Na kwa mantiki hiyo kama Tabora ilijisifu kwa kupanda takwimu ya kufaulisha basi ilikuwa ikifanya hivyo ndani ya wajinga.Naamini kwamba hata kama ukichukua kundi la wajinga na kuwapa mtihami pekee, lazima apatikane aliye bora kati ya hao wajinga, na inawezekana Tabora imo ndani na ilikuwepo katika kufanya vizuri kati ya mikoa mibovu katika elimu Tanzania, hapo hatuwezi kujisifu hata kidogo.

Kuna kunashindikana nini Tabora kushika nafasi ya 1, 2 au ya 3 kitaifa ama kuwepo katika 10 bora kitaifa?.Nafikiri ndo limewapelekea wanashinyanga kuweka mkakati wa "Operation Okoa Shinyanga ni Lazima", Ili kuondokana na aibu hizi za kila kitu shinyanga ni ya mwisho wakipokezana na walina asali(Wanatabora), kweli ni aibu.
Hapa lazima tujiulize sote, ama kama wadau, wazalendo,na wasio wanatabora, kwamba kila kitu kinawezekana kama dhamira na mikakati thabiti ikiwepo juu ya jambo fulani.Kwani mikoa inayokuwa inashika 10 bora kuaznia ya 1 mpaka ya 10 ina kitu gani?,je ina mikakati ipi inayotumia mpaka kushika nafasi hizo ambazo mkoa kama wa Tabora hawawezi kutumia mikakati hiyo na kujifunza ili kuinua Elimu mkoani Tabora?, je nani alaumiwe?.

Mwaka 2004, jumamosi ya tarehe na mwezi nisiokumbuka, nilimuuliza swali mojawapo mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Nzega, Lucas Seleli, katika mkutano alipotembelea kijijini kwetu Idala ambapo ni umbali wa Kilomita 6 hivi toka Nzega mjini.
Nilimuuliza swali kwamba"Je, yeye kama mmoja wa wabunge wa mkoa wa Tabora, wana mikakati gani kuinua mkoa wa Tabora kielimu kuondokana na adha ya kuodorora kwake?, Ama je yeye kama Mbunge, huwa hawaoni aibu bungeni wanaposikia na kutangazwa kwamba mkoa wa Tabora umeshika nafasi ya mwisho?".

Nakumbuka jibu alilonijibu mheshimiwa Seleli wakati wa kujibu maswali yaliyoulizwa, ni kwamba moja alijibu kuwa ni kweli walikuwa wakipata aibu kubwa kweli kutoka kwa wenzao ambao mikoa yao inapeta kwa kuwemo kwenye 10 bora.
Ila jibu la mikakati ipi walikuwa nayo kama wabunge kushughulikia elimu mkoani humo, kwa kweli sikumbuki kabisa, labda kwa vile lilikuwa si jibu toshelevu na sahihi zaidi, ingawa laweza lilikuwa mojawapo ya majibu ya kiasi cha kuwa sahihi,mimi sikumbuki hata kidogo.Kwa maana nyingine sikuridhika na majibu ya swali langu na ndo maana sikuwa na haja ya kulikumbuka.
Hawa ndo wabunge wetu, ambao ndo wangelikuwa wa kwanza na mstari wa mbele kulia na kuomba ama kuishawishi serikali kila mara na bila kukoma ili mkoa huu uwezeshwe na kuboresha elimu mkoani humu wakisaidiana na wadau mbalimbali wa Tabora kama nilivyoanisha hapo mwanzo.

Kwangu binafsi, siwalaumu wabunge pekee katika swala hili ambao naweza kuwalaumu na kusema wanawajibu pekee wa kuimarisha elimu Tabora.Isipokuwa ni wajibu wa kila mtu mzalendo na mzawa na mwenye mapenzi mema na mkoa wa Tabora, hii iwe akiishi ndani ya mkoa huu au nje ya mkoa huu ili mradi yumo katika makundi niliyoyataja ya wanatabora.

Na nina imani kwamba wapo watu wa kada mbalimbali ambao ni wazawa, wenye asili na wazalendo wa mkoa huu ambao wako nje ya mkoa huu na wana amana nzuri tu ya mali za kipesa na kifikra, wasomi na wanazuo wazuri tu, lakini wamejisahau na kuusahau mkoa wao, kana kwamba walifanya mabaya walikotoka na pengine labda walikosea kuzaliwa kule na wangezaliwa labda mikoa mingine.

Tutasemaje hapa kama kweli watu wa kada mbalimbali wapo na wanashuhudia jamii yetu inaangamia kwa ujinga na hakuna anayepata uchungu hata wa kusema kama mimi hapa, ingawa najilaumu kwa kuchelewa kukumbushana haya.Na sina uhakika kama yatawaingia wahusika popote wasomapo maoni yangu haya ama nitakuwa napiga ngoma na wakisikia lakini wasielewe na kupuuzia.

Hata hivyo tatizo ninalolifahamu mimi kwa ndugu zangu hawa wanatabora, wanatabia ya kutokujali wanakotoka.Mwanatabora akisha fika pale alipo, mfano kule Dar es salaamu sehemu kama Msasani, Oysterbay,Mbezi Beach na sehemu kama hizo kwa mikoa mingine, basi yeye huwa hakumbuki kabisa tena na hana haja na jamii anakotoka, jambo ambalo ni tofauti na jamii kama za wachaga na ndo maana kilimanjaro hapo ilipo imefikishwa na watu wake kuupenda mji wao na kupenda na kuuendeleza kwa nguvu zoote mkoa wao.

Mwanatabora yeye hufikia hata kukana kwa utambilisho wake kwamba anatokea kati ya mikoa hii ya Tabora ama Shinyanga ama Mwanza awapo katika ustaraabu mbalimbali hata kama kuna uewezekano wa kutambulika kiasili kwa kuwapo vyama mbalimbali vya kimkoa, kikanda kama ilivyo katika vyuo vikuu nchini.Walio wengi huwa hawajitambulishi katika vyama vyao vya kinyamwezi ama MWASHITA(Mwanza, Shinyanga na Tabora), na hawako tayari kushiriki katika jambo lolote ndani ya vikundi hivi, na kama nasema uongo muulizeni Mheshimiwa Mbunge wa Maswa wa sasa, John Shibuda alikuta nini katika Chama cha MWASHITA, chuoni Mzumbe pale alipoalikwa kuwa mgeni rasmi 2004 katika moja ya sherehe iliyoandaliwa na chama hiki.

Jamani hii ni tabia gani?, unasahau jamii yako, asili yako, utamaduni wako na hata lugha mama?, wewe ni mtu wa wapi?.Huu na hawa ndo wanaoitwa 'Mabukanya" kwa maana moja ya kuwa na uroho wa kipekee na ubinafsi.Kwa nini usikumbuke kwenu? nyie mna nini? hamuoni wenzenu wanavyopafagilia kwao kama akina iwe?.Aisee inatisha na hakuna mfano.
Acha nisitoke kwenye mada yangu ya leo na hili si tatizo kubwa kama mmenielewa wahusika mmenielewa ninachobwata hapa.Cha msingi ni kwamba wanatabora kuweni na moyo wa kujionesha, kujivunia na kuwa na mapenzi mema ya kukumbuka mkoa wenu katika suala zima la Elimu.

Pengine kuna haja ya kuweka makakati wa Operation Elimu Tabora ni Lazima(OETL) Kwa maana kwamba kuwa na malengo ya makusudi kabisa ya kuundeleza na kuboresha Elimu mkoani Tabora kwa njia yeyote ile na mkakati wowote ule ili mradi Elimu Tabora Tabora inapanda, Vinginevyo tutajikuta wapagazi wa mikoa mingine kwa kuwa sisi tu wajinga Kielimu.

Bado wenye elimu zao ndo watakuwa watawala ndani ya mkoa wetu hata kama panahitajika awepo mzawa kwenye nafasi hiyo,mpaka kwenye uwenyeviti wa vitongoji watu toka mikoa mingine watashika nafasi hizo kama wanatabora watabaki nyuma kielimu na kasi yenyewe ndo hiyo ya kutupa jongoo na mti wake.

Pengine tutajikuta kila mkoa una mikakati na matarajio ya kujenga chuo kikuu hata kama kwa miaka 15 ijayo lakini sisi kwa mwendo huu, wala hatuna habari.Ndio tunahangaika na elimu ya shule ya msingi tu nayo ni mbovu seuze chuo kikuu.

Ninavyoona mimi kuna haja ya wasomi wetu, matajiri wetu, mashirika ,kada mbalimbali wa mkoani Tabora ama wenye uzal;endo na mkoa huu tukae na kukubaliana kwamba , mosi tatizo ni nini katika elimu yetu Tabora, pili tufanye nini kama tutapata tatizo,tatu, tuanzie wapi na vipi katika tatizo hilo, je rasilimali zipo pamoja na wataalamu wa elimu wazalendo?, pesa? na kama havipo tuweke mikakati ipi ili kupata rasilimali(resources) hizo ili kufanikisha program yetu ya OETL, Swala kubwa ni kuwa tunataka sasa na tunaelekeza nguvu zoote kwenye kuwekeza Elimu kwa jamii yetu hakuna kitu kingine hata kama kwa miaka yapata 30 hivi potelea mbali matunda tutavuna huko mbele.
Kwa mfano tunaweza kujiuliza maswali hayo tukiwa na mikakati ya kuweka OETL kwa miaka mitano mitano kuwa kila wilaya iwe na shule ya sekondari moja ya kuaznia kidato cha 1 mpaka 6, halafu mitano mingine kila Tarafa iwe na shule ya sekondari kuanzia kidato cha 1 mpaka cha 6, na baadae hata kijiji.Na mwisho na baade tena tunaweka mipango wa miaka kumi kumi kwamba mkoa wa Tabora uwe na chuo kikuu ifikapo mwaka 2030, HILO linawezekana kwa kabisa kwa m,ipango mahususi na ya makusudi kwa ushirikiano wa pamoja.


Si hivyo tu, mipango hii iende sanjali na kuboreshaji elimu kwa ujumla kwa kusimamia elimu yetu ikiwemo kamati na tume mbalimbali zitakazoundwa kwa mujibu wa wadau woote.Kama ikibainika kuna viongozi ama mtu yeyote aliyepewa dhamana ama na sisi au na serikali akichezea elimu mkoani mwetu basi tuwe wakali na hatuna budi kumkataa kwa vile anatuletea ugonjwa mbaya wa milele wa ujinga na upumbavu wa kutokuwa na elimu bora.

Kwa mpango huu inawezekana kabisa kama wakubwa wetu wengine wakiweka hata harambee, chakula cha jioni ya mara moja hata kwa mwaka kukutana na nakuchangia mali za akili, fikra yakinifu, vifaa na pesa ili kuinua elimu mkoani mwetu.

Ndugu zangu hakuna atakayekuwa na uchungu na mkoa wetu kama sisi wenyewe hatuujali na kwa kudorora kwake katika nyanja zoote hasa kielimu kwani tukiwekeza kwanza kwenye elimu na mambo mengine yatafuata, vinginevyo tunaiweka rehani jamii yetu kuwa watumwa wa milele kwa kutokuwa na elimu bora

Naongeza tena cha msingi tuache ubinafsi, uroho wa kipekee na tamaa za kujidai kutokujali jamii yetu, huo sio ujanja ni ushamba na ujinga katika jamii iliyoelimika.
Kwani hatuoni au huwa hatusikii kutokana na mifano wa mikoa mingine unakuta wanaitishana kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwamba wana mkoa fulani wanatakiwa wakutane tarehe fulani na mahala fulani, agenda ni kujadiliana jinsi ya kutatua matatizo ya mkoa huo, moja likiwa ni elimu, na hapo hapo unasikia na mgeni rasmi atakuwa mheshimiwa fulani(Labda waziri au mkurugenzi wa kampuni fulani), kwa sisi hilo haliwezekani?, je hawa waheshimiwa sisi hatunao?, au hawatambui hilo?.

Jamani tujifunze basi kwa mifano na vitendo kama hivyo juu, kuinua elimu yetu Tabora.
Hivi nyie wenzangu tukishapita sisi ambao angalau tuna hicho kielimu au tumeshapata kidarasa bora kiasi kuliko wenzetu wa sasa na jua likatufika saa 10, hiyo jamii inayopata elimu mbovu na hakuna uwiano wa wasomi wengi mkoani humo kwa nyakati hizo nani atawasikiliza katika matatizo yao kwa vile watakuwa nyuma nusu saa kielimu kuliko mkoa wowote?.

Namalizia, jamani wasomi wetu(maprofesa wanatabora, madaktari wa falsafa wanatabora, wenye shahada za uzamili, shahada za kwanza, diploma na wenye vidato wanatabora) mko wapi kuinua elimu mkoani mwenu?, amkeni kumekuchwa, tunaachwa na gari la utandawazi wa elimu.Jamani wenye mali zenu za kipesa na maarifa wanatabora mko wapi kuchangia elimu yenu ili iboreke katika jamii ya wanatabora?, amkeni kumekuchwa, tunaachwa na gari la utandawazi wa elimu.

Jamani waheshimiwa akina Prof.Juma Kapuya, akina spika wa standards and speed, ioneshe speed yako hata mkoani kwako na jimboni kwako amabko kuansekemkan kuna umaskini usio na mfano, je unasimamia kiwango gani wakati kiwango(standards) cha elimu mkoani kwako kimedorora?, weka kiwango hicho kwa wanatabora, kila kitu kitawezekana.Jamani waheshimiwa wabunge akina Dr.Msekela, Lucas Seleli mko wapi,madiwani wetu mko wapi? wekeni mikakati kuboresha elimu ya wanajamii wa tabora, nyie ndo tumewatuma mkahemee bungeni ni pamoja na elimu bora.je na nyie wananchi je mko hange hange kwa hili la elimu au ndio mshika shuka na ngoma za waswezi na uyeyebila kujali elimu?, amkeni jamani gari la utandawazi hilooo,linapita litatuacha.

Hitimisho, "Haya jamani Kasi mpya ya kusahau kwenu", mtanikumbuka hata kama nitakuwa sipo duniani hata kwa kifikra zangu hizi".

1 Comments:

At 4:25 AM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Tabia ya "wasomi" kwenda Dar na kusahau mikoa waliyotoka ni mbaya sana. Wabunge nao huwa wanakimbilia huko Dar. Dar yenyewe huwa tunaona ndio Tanzania. Utaona watu wanaongelea maendeleo ya nchi kwa kutazama yanaotokea Dasalama.

 

Post a Comment

<< Home