Sunday, March 12, 2006

TANZANIA na ushiriki wake ndani ya jumuia ya afrika mashariki:
• Tulijiandaaje kuingia ndani ya EAC?
• Uwezekano wa kuwa wasindikizaji ni mkubwa!

Ni kwa mapenzi mema ya waliokuwa marais, wawili wameshastafu na kuachia madaraka kwa mujibu wa katiba za nchi zao na mmoja bado yupo madarakani, ambao jumla yao ni watatu ndani ya nchi ya Tanzania, Kenya na Uganda, kung’amua kuanzisha na kuifufua tena Jumuia ya Afrika Mashariki yaani EAC(East African Community).

Marais hao ni Benjamini William Mkapa wa Tanzania, Daniel Arap Moi wa Kenya, na Yoweri Kaguta Museveni waUganda ambaye mpaka sasa anaendelea kuwa rais wa Uganda. Maamuzi yao yalikuwa sahihi kabisa kuanza tena kwa EAC baada ya kuvunjika hapo mwaka 1977, na ninafikiri baada ya mwaka kama mmoja hivi au 2, kuvunjika kwa EAC ya kwanza, Tanzania ikaingia kwenye vita na Uganda.

Kwa maana nyingine twaweza kusema kuvunjika kwake kulikuwa na sababu moja au zaidi ya moja ambayo hali haikuwa nzuri ndani ya jumuia hii mpaka kupelekea kuingia vita baada ya mwaka mmoja tu.
Kwa maana hii, tusiombee tena historia ijirudie katika jumuia hii, kwani katika umoja au shirikisho ama jumuia kama hii, kwaweza kuwa na faida nyingi tu ndani ya jumuia lakini kunaweza kukatokea vile vile sababu moja hasi inayopelekea kuvunjika kwa jumuia au shirikisho husika.Hilo tuombe Mungu na hatuombei tena itokee, ila tu Mungu aibariki jumuia yetu hii ya EAC tusonge mbele.Katika kuundwa kwa jumuia mpya hii hapo mwaka 2001, kuliorodheshwa faida nyingi tu ndani ya Jumuia hii mpaka wakaridhia hao marais kuundwe tena EAC, na uhakika nilionao ni kwamba hata rais wa sasa wa Tanzania Jakaya Kikwete alikuwa ni mmoja wa waunda ama washiriki wa mchakato mzima wa kuanzishwa kwa EAC kwa mara nyingine, pale alipokuwa kama waziri wa nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania.
Na hii ndio maana imepelekea rais Kikwete kuiundia wizara mahususi jumuia hii kama Wizara itakayoshughulikia mambo yote yanayohusiana na EAC, na waziri wake akawa Andrew Chenge, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa aserikali ya awamu ya tatu. Hilo ni jema

Hata hivyo sihitaji katika mada yangu ya leo kuorodhesha faida na malengo yoote iliyodhamiria kuyafanya jumuia hii ndani ya wananchi wake, yapo mengi kwa kweli na mojawapo muhimu ni hili la ushuru wa forodha ambalo linatoa fursa katika masuala yoote ya ushuru katika biashara ndani ya nchi hizi zinazounda jumuia ya Afrika Mashariki.

Mada yangu ya leo inajikita katika ushiriki wa Tanzania ndani ya EAC.Hivi kweli nitakuwa nje ya mstari nikiuliza kwamba, “Je Tanzania ilijiandaa kuingia ndani ya jumuia hii kweli? au ilipata shinikizo Fulani toka pande zingine na si utashi wake?, Je Tanzania kama ilijiandaa, sasa imejiandaaje kusakata kabumbu (mpira wa miguu) ndani ya uwanja wa EAC, kati ya timu ya Kenya na Uganda?.

Hivi kweli timu ya nchi yetu iliandaa wachezaji wa timu nzima ya kucheza ligi hii lakini ligi ya maendeleo kwa wananchi wa Tanzania ?, Je wachezaji waliandaliwa kwa muda gani?, je wana vifaa vyote vya mchezo kama viatu vya mpira vinavyostahili kwa kuchezea mpira au hakuna?.
Maswali yaweza kuwa mengi, lakini haya yanatosha kujadili ninachopata wasiwasi wa Tanzania ndani ya EAC.

Pengine wasiwasi huu ni wangu pekee.Sasa kama wadau wote wa jumuia hii hasa kwa watanzania hebu tufikirie sote.Je utasemaje Tanzania ilijiandaa kuingia ndani ya EAC, wakati tukiangalia kwa upande wa rasilimali watu inaonekana Tanzania iko nyuma kwa kila nyanja hasa kwa watalaamu mbalimbali ukilinganisha na washirika wenzetu wa EAC?

Mfano kwa kila hali, kwa kila takwimu kwa upande wa wahitimu mbalimbali toka vyuo ama taasisi za elimu ya juu inasemekana, Tanzania kwa mwaka inatoa wahitimu 10,000 pekee,wakati Kenya na Uganda wanatoa wahitimu kwa mwaka 40,000, sawa na uwiano wa moja kwa nne, yaani 1:4, amai palipo na wahitimu 5, mtanzania ni 1 tu.

Pengine hata hayati baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliliona hili miaka 45 iliyopita.Katika hotuba yake Mei Mosi, 1961, yaani kabla ya miezi saba tu Tanganyika ipate uhuru na yeye Mwalimu akiwa Waziri Mkuu wa Tanganyika wakati huo. Mwalimu katika hotuba yake hiyo alibainisha kuwa Tanganyika ilikuwa nyuma sana kielimu ukilinganisha na nchi za Nigeria na Ghana. Bado aliongeza pia kwamba vile vile Tanganyika tulikuwa nyuma sana kielimu ukilinganisha na nchi zetu jirani za Kenya na Uganda kwa miaka hiyo ya 1961.

Mimi binafsi hapo napo ndio bado najiuliza kama Mwalimu aliyasema hayo na hali ya Tanganyika kuwa nyuma kielimu, na bado ilipiga masafa mpaka kuwa Tanzania ya sasa takribani miaka 45 sasa, bado sisi tuko nyuma kielimu ukilinganisha na wenzetu, je huo ushiriki ndani ya EAC utakuwaje?.

Ushiriki utakuwaje kwa maana ya kama timu ya mpira kama hawa wenzetu walijiandaa tangu miaka hiyo ya yapata 45 iliyopita, kwa kuwaandaa wachezaji( watalaamu wa fani mbalimbali) kielimu, sisi tutawezaje kushindana nao?, je tutawezaje kupata uwiano wa watalaamu katika nyanja mbalimbali panapotokea mgawanyo wa kazi ndani ya jumuia hii kwa 1:4?.
Isitoshe basi mpaka sasa bado tunaimba wimbo ule ule wa Mwalimu Nyerere wa mwaka 1961, mei mosi kwamba Tanzania tuko nyuma kielimu ukilinganisha na jirani zetu na washirika wenzetu ndani ya EAC.Je tumejidhatiti vipi kwa upande huu wa kuboresha elimu na kwa kutoa wahitimu wingi zaidi kwa mwaka ili kwenda sambamba na wenzetu?

Hapa hatuoni kwamba, hata ukichukua hesabu za yamkini(Probability), katika uwiano wa wahitimu , na hata wa watalaamu tulionao sisi na wenzetu tangu miaka hiyo, sisi tutakuwa na nafasi ndogo sana ya moja kwa 5 palipo na watu 5 na wenzetu wanakamatia yamkini ya nne kwa tano kila mmoja hasa pale panapotokea mhitimu hata mmoja anahitajika kwa kazi Fulani?, jamani hii ni aibu. Na ndio maana nikauliza je Tanzania tulijandaa kweli kuingia EAC kwa utashi wetu wenyewe au kwa shinikizo toka upande mwingine.

Haya upande wa madaktari waliopo na wahitimu wa fani ya udaktari kwa mwaka inasemekana Tanzania tuko nyuma .
Ukija kwenye suala la polisi, Tanzania kwa upande wa askari wa kulinda usalama wa raia sisi tuko nyuma kwa kuchukulia askari polisi mmoja alinde au awahudumie katika ulinzi watanzani kazaa, vivyo hivyo kwa madaktari na wagonjwa.

Pia Tanzania, sarafu yetu iko chini zaidi kuliko ya Kenya, labda hapa Uganda tunawazidi na sisi.Bado hata maslahi ya wafanyakazi au wawakilishi kama wabunge Tanzania inatoa maslahi kidogo kulinganisha na washirika wenzetu ndani ya EAC, na ndio maana wabunge wetu waliling’amua hili na kuanza kudai maslahi yanayolingana na wabunge wenzao wa nchi hizi EAC.
Lakini labda walipopotoka wabunge wetu, ni kwamba wangedai maslahi ya kwao pia na y a walimu, madaktari na wafanyakazi wengine kwa maana na hoja hiyo hiyo ya kwamba maslahi hayo ni madogo ukilinganisha na wafanyakazi wa washirika wetu ndani ya EAC.

Kutokana na niliyoeleza hapo juu, mimi binafsi huja na maswali ya.Je kweli kama watanzania hatuna wahitimu wa kutosha katika fani mbalimbali, je tutawezaje kucheza kabumbu la ajira kwa wahitimu wetu hawa wachache kiasi kwamba hata hapa kwetu hawatoshi, na bado inawezekana wakawa wahitimu sio compentent.
Je hatuoni hapa Tanzania tunaweza tukawa wasindikizaji tu, na wapagazi wa kubeba mizigo ya wenzetu ndani ya jumuia hii katika sekta yeyote ukianzia na kilimo kwa wakulima mpaka sekta ya uchumi wa kibiashara na hata katika ajira mbalimbali za kampuni binafsi na uwekezaji kwa ujumla..

Labda niulize tena ,je Tanzania tumejiandaaje sasa kwa kuwa na watalaamu wa kutosha katika kila nyanja iliyoanishwa katika maadhimio ya kwamba mambo Fulani ndio yatakuwa kipaumbele mfano hili la ushuru wa forodha?.Je mfano kukitokea wanahitajika watalaamu wa masuala ya manunuzi (Procurement) yaani procurement professionals, au professional buyers, je Tanzania tunao wahitimu na watalaamu hawa wa kutosha?, na je kama wapo wanaweza kuhimili ushindani wa utalaamu wao na wenzetu wa Kenya na Uganda?.
Hii natoa mfano tu wa upande mmoja na bado mfano kama huo kwa fani zoote na fani mbalimbli nchini.

Kwa maana nyingine inabidi tukae na kujipanga upya kama sio kujipanga upya basi tuzidi kujiimarisha na kuboresha mikakati tuliyokuwa nayo kukabiliana na ushiriki wetu ndani ya Jumuia yetu kwa kasi ya aina yake na kw kiwango cha juu kabisa na kwa umahiri wa aina yake. Hata hivyo, kama tulikuwa bado basi tuanze kuchachalika kwa mambo niliyoanisha hapo.Na kama tuna mikakati yeyote, basi wenzetu wakiwa wanatembea sisi tuwe tunakimbia ili kwenda sambamba ndani ya EAC, kwa maana kwamba tusije tukajikuta tunasindikiza kila kitu na kushangilia ushindi ukienda Kenya na Uganda na sisi tukiambulia masalia na chuya zilizoachwa na wenzetu baada ya kuchuka mchele ulio safi na bora.

Ni wajibu wa kila mtanzania, na serikali yenyewe kuzidi kujiuliza masuala yote na maswali yoote niliyoyabainisha hapo juu, ila mimi hofu na wasiwasi wangu bado ni mkubwa sana kwa Tanzania kuhimili kishindo cha mikikimikiki ya jumuia hii, kwani wenzetu wanaonekana wako juu na walijiandaa kweli tangu siku nyingi.

Cha msingi hapa na ninatoa ushauri wangu kwa serikali kupitia wizara ya ushirikiano wa jumuia ya afrika mashariki chini ya waziri wake Andrew Chenge, kuwapo kwa elimu ya ujumla kwa kila mdau, raia, mzalendo wa Tanzania hii, aliyeko ndani na nje ya nchi yetu, juu ya faida, na dhana nzima ya kuwapo kwa Tanzania kwenye jumuia hii. Elimu itolewe kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama redio, televisheni, magazeti na hata majarida mbalimbali kuuelimisha umma kwamba Tanzania tupo ndani ya jumuia ya EAC, kwa ajili hii na hii, na faida zake kubwa ni hizi na hizi, na sasa tuna mikakati hii na hii, na kwa kila mtanzania ili afaidike kwa kupitia jumuia hii yeye kama yeye anatakiwa ajitahidi kufanya hiki na kile ili kupata matunda na faida ya moja kwa moja kwa mwananchi.

Dhana hii itamuwezesha kila mtanzania kuwa na juhudi zake pekee katika ushiriki ndani ya jumuia ya EAC kama atapata elimu ya kutosha kuhusu jumuia hii, na siyo ibaki uelewa wa wasomi ama serikali kama serikali katika utawala kwamba tunafaidika ndani ya jumuia ya afrika mashariki kwa njia hii.Hapa itakuwa si uwazi na ukweli bali utakuwa ni usiri na kificho.

Serikali pia kwa kupitia wizara yake uwepo uwezekano wa kuweka kama mada au kama mtaala Fulani mashuleni wa elimu ya Tanzania ndani ya jumuia ya afrika mashariki na faida zake ili kuwajenda wanaosoma uzalendo na elimu ya ujumla kuhusu na kuwa na ari ya kufanya kazi kwa ajili ya kukabiliana na ushindani ndani ya EAC.
Dhana hii takuwa sawa tu, kwa vile hata huko nyuma tulivyosoma sisi, mbona kulikuwapo na mada za Tanzania ndani ya Jumuia ya Madola, Tanzania ndani ya nchi zisizofungamana na upande wowote. Cha msingi hapa ni kuweka mtaala huu kwenye somo linaloendana na maarifa ya ushiriki wa Tanzania ndani ya jumuia ya afrika mashariki.

Pengine kuwepo ukweli kwa kila raia hasa wananchi wa kawaida kuhusu jumuia hii kwa Tanzania kutawafanya kujitahidi katika eneo moja la uzalishaji na kuweza kushindana na wenzao wa Kenya na Uganda.

Mfano katika kilimo, wakulima wakijua na kupata ufahamu wa kina kuhusu Tanzania kuwepo kwenye jumuia hii na faida zake ni hizi kwa watanzania, wakulima hao hao wataweza kuweka jitihada za kuwa na kilimo bora na uzalishaji wa mazao bora ili kushindana kwenye soko la pamoja ndani ya jumuia hii na kama tu serikali nayo itawawezesha katika kilimo hicho.

Elimu hii itawawezesha hata yule mwananchi wa vijiji kama vya Idala, Uchama Nzega, Ilagala-Kigoma, Kamachumu-Kagera,Makanya-Same(Kilimanjaro), Mlali kule wilaya ya Mvomero-Morogoro kuwa na uelewa wa kina na pindi unapomuuliza Je wewe kama mwananchi unafaidika vipi na Tanzania kuwepo katika jumuia hii, Basi jibu litoke toshelevu na lisilo na jibu la sijui, ama serikali ndio inajua. Hapo tutakuwa hatujafanya kitu kuwepo kwetu ndani ya jumuia hii.

Basi na tuwe na imani ya matendo ya kwamba Tanzania tutafaidika na tutacheza ngoma ile ile waichezayo wenzetu ndani ya jumuia hii. Ila kuna uwezekano wa kuwa wasindikizaji tusipojidhatiti kwa mambo niliyoyabainisha hapo juu. Hebu tusubiri tuone.

2 Comments:

At 3:44 PM, Blogger Frank said...

inabidi tujiandae lasiivyo tutashindwa kama mwaka 1977.

 
At 5:21 AM, Blogger mzee wa mshitu said...

Kusindikiza hilo ni suala la wazi sababu katika kila nyanja tuko nyuma iwe katika elimu, viwanda na au uchumi kwa ujumla, kimiundombinu na kwa maana hiyo huu mkataba utakaoanza kutumika hivi karibuni eti kuruhusu mawakili wa Kenya kuvuka mipaka kutasababisha crisis kwetu.

Just imagine kwetu wapo mawakili wasiozidi 3,000 wao wapo zaidi ya 10,000 sasa hapa jumuiya hii itakuwa kwa maslahi ya nani bila shaka jibu linajulikana na hatimaye matokeo yake sote tunajua hakuna atakayekebalika kudhulumiwa.

Huo ni mfano mdogo yapo maeneo mengi sana ambayo tupo nyuma ambapo tukiruhusu ushirikiano 'feki' kama huu tutakwisha.

 

Post a Comment

<< Home