Saturday, April 22, 2006

Fikra Pevu Kwa Wasomi Wetu Ni Ndoto Isiyotafsirika!

Tunaambiwa kwamba miaka ya 1961 kuja 1970, nchi kama Korea, na zile za mashariki ya mbali na hasa zile za bara la Asia zilikuwa sawa kiuchumi na Tanzania. Kuanzia pale nchi hizo ziliekeza nguvu na uwekezaji katika elimu kwa mbinu yeyote ile ili mradi tu watu wake wapate elimu ya kutosha na iliyo bora zaidi. Na ndio maana mpaka sasa watu hao wako mbali sana kimaendeleo wakiwa mbali sana katika maendeleo hasa ya kisayansi na teknolojia. Hilo ndio zao la kuwekeza katika elimu, kwani wao waliona bora kuutafuta kwanza ufalme wa elimu na mambo mengine yangefuata baadae.

Ila kwa nchi yetu Tanzania hilo hatukulitambua na mpaka sasa bado hatulitambui mpaka sasa nchi kama Botswana zinatuacha nyuma kwa maendeleo, ni sababu hizi hizi za kujisahau kuwekeza katika elimu kwa nchi yetu ndio inasababisha madhara makubwa kama ya kuwepo njaa kali, kuwepo kwa umaskini wa kutupwa kwa wananchi, kuwepo kwa kilimo mfu kwa wakulima na kilimo huku tukiimba Tanzania inategemea asilimia kubwa katika kilimo, yaani kilimo ni uti wa mgongo wa nchi yetu, kuwepo kwa taifa tegemezi kwa mambo mengi tu.

Hata pale tunapoona kuna umuhimu wa kuwekeza katika elimu, bado tunaweka mipango mfu isiyotoa tija na elimu bora kwa wale wanaoipata. Kuwekeza katika elimu ni pamoja na kuiweka elimu hiyo katika mazingira bora yanayoendana na mabadiliko ya dunia, inayoendana na utamaduni wa nchi husika, inayozingatia utaifa wa nchi husika ili kuwajengea watu wanaoipata elimu hiyo ari ya kuipenda nchi yao na kupendana wao kwa wao yaani kuwa na uzalendo. Vinginevyo kuwepo kwa elimu inayokuwa na mitaala tata ya kimagharibi pekee, siyo kipimo cha kupanda kwa elimu na kuboreka kwa elimu, hiyo itakuwa ni kujenga taifa lisilojiamini, taifa lisilo na utamaduni na utaifa kama nchi zingine tunazoziona zinazingatia mambo kama hayo.

Elimu bora ni ile inayomfanya mwenye elimu hiyo kuwa mtu mwenye kujenga fikra pevu, iliyokomaa, isiyo tegemezi, elimu inayomfanya mtu mwenye elimu hiyo kujiamini na kitu anachokifanya kutokana na elimu hiyo aliyoipata. Usomi na msomi makini kama walivyokuwa akina Plato, Aristotle ni ule unaozingatia uzalendo wa nchi ya msomi husika, msomi anayetambua utamaduni wake, msomi mwenye kujenga fikra za kuweza kuendeleza nchi yake.

Hata hivyo usomi wa kufikiria ajira pekee si usomi unaohitajika katika maendeleo ya nchi hasa nchi zinazoendelea. Ajira ni matokeo ya kuwa na elimu hiyo, tena elimu bora, si elimu ya kukati, na kukopi. Elimu inaweza kutengeneza ajira kama elimu hiyo na watu walio na elimu waliwekewa mazingira ya kujitegemea na mazingira mazuri ya kuwepo kwa elimu hiyo toka kwa serikali husika katika nchi husika.

Binafsi, nimekuwa nikisoma makala, maoni ya watu mbali mbali katika magazeti ya hapa nchini.Waandishi wengine wamekuwa wakijikita kwa kuuliza inahitajika vitu gani ili kujenga hekalu imara?, je ni elimu?, je ni ajira nyingi kuwepo ?, je kukua kwa uchumi kwa nchi, na uchumi huo ukue vipi na kwa njia zipi?.

Katika makala hizo, mmojawapo ni mwandishi Padri Privatus Karugendo, amekuwa akiibua mijadala ya maswali kama hayo hapo juu. Katika gazeti la Rai toleo namba 654 la april 20-26, Karugendo anaadika makala yake inayosema”Elimu yetu: Mitaala bado ni ya kikoloni, tangu mwanzo lengo ni kutufanya tusifikiri.”

Mimi binafsi naungana moja kwa moja na mwandishi Karugendo kwa makala yake hiyo. Lakini bado nina maswali vile vile ya kujiuliza kutokana na makala ya mwandishi huyu. Kwamba ni kweli mitaala yetu bado ni ya kikoloni inayotufanya tusifikiri?, na kwa hiyo anapendekeza kuwepo na mtaala wa somo la falsafa ili kuwafanya wasomi wetu na wanaopata elimu hiyo waweze kuwa wadurusaji, wenye kufikiri kwa undani kila kitu kinachofanyika hapa duniani, kwamba kwa nini hiki kiwe vile na kwa sababu gani hiki kiwe hivi, na njia ipi itumike kukifanya kitu kiwe vile. Hilo ni jambo zuri na kama kweli watu waliopewa dhamana ya kusimamia elimu yetu watakuwa wanasoma makala za mwandishi Karugendo, na wakapuuzia maoni yake basi kweli tutaamini elimu tulionayo inatufanya tusifikiri.

Labda pengine naweza kujiuliza, Je Tanzania, kuanzia kwa mwananchi wa kawaida, aliyepata kukanyaga japo darasani, akapata elimu ya kufuta ujinga, wasomi wetu wakiwemo wenye vidato mbalimbali, wenye stashahada za kawaida na za juu, wenye shahada za kwanza, wenye shahada za uzamili na uzamivu(PhD), maprofesa wetu na wadau wengine wa elimu nchini, je hakuna hata mmoja aliyekuwa na mwenye mawazo kama ya Mwandishi Privatusi Karugendo kuhusu ufeki wa mitaala yetu katika elimu yetu inayoegemea fikra za kiamgharibi zaidi na tegemezi, tangu enzi hizo za 1961, tangu tulipopata uhuru?.
Je hakuna hata mtu mmoja katika jopo la watu wanaopewa dhamana ya kusimamia elimu yetu nchini ambae huliona hili, hata kulifikiria basi, na kulisema japo mara moja tangu miaka hiyo ya uhuru mpaka sasa miaka 45, umri wa mtu mzima huu. Yaani hakuna anayelitambua hili kwamba mitaala yetu ni tegemezi zaidi, ni mitaala inayotufanya tusifikiri kwa mujibu wa Karugendo?. Inawezekana au isiwezekane.

Je ni sababu hizi hizi za mitaala ya kikoloni, inayotufanya tusifikiri ndio iliyotufanya, na inayoendelea kutufanya tusifikiri mitaala yetu ni ya kikoloni?, Je ina maana hata wasomi wetu niliowataja hapo juu nao wana usomi usiokuwa wa kufikiri na fikra pevu kwa vile wanaelimu ya mitaala ya kikoloni inayowafanya wasifikri hivyo?.

Lakini mbona napata wasi wasi hapa kuwa hapa Tanzania sasa tuna watu wenye shahada za uzamivu wengi tu, maprofesa wengi tu wa fani mbalimbali, na makademishani wengi tu, je katika shahada ya uzamivu(PhD), si kuna somo hasa linaloitwa la falsafa, yaani somo la fikra zaidi kuliko elimu zingine za kutegemea kuambiwa kitu hiki kiko hivi na hakuna sababu ya kujua undani wake.

Je hawa nao waliopata hilo somo na kuwa na PhD, hawana msaada kwa nchi yao kuling’amua hili la mitaala za kikoloni na kwamba kuna umuhimu wa kuwepo kwa somo hili katika elimu yetu nchini?, au hata hizo PhD, zina mitaala ya kikoloni zaidi kuliko falsafa yenyewe ilivyo?. Lakini hata hivyo falsafa ni kitu kinachomfanya mtu ajiulize maswali ya uhalisia kuhusu kitu fulani na wakati huo ni lazima atafute majibu yake, sasa kwa wasomi wetu hilo halipo?.

Mimi ndio utata wangu uko hapo na haniingii akilini kabisa, kuona elimu yetu nchini bado inachezewa makida makida tu, na kubadilishwa mitaala kwa majaribio ya hapa na pale.Basi si kuwepo na tume yenye wataalamu wa kuchambua, kufanya utafiti kuhusu elimu inayotolewa nchini inayoendana na mazingira yetu na ya kimataifa, kama wataalamu hawa hawapo basi si ni bora serikali ikaingia gharama ya kusomesha watu kwa ajili ya utaalamu huo wa kutunga na kuchakata mitaala ya elimu ya nchi yetu.

Nionavyo mimi kwa vile mitaala hiyo tuliipokea toka kwa wakoloni hawa, tukaikubali, tukaendelea nayo, na tukaiendekeza ya bila kuitafakari kwa undani mpaka sasa, basi na tumekwisha.

Tumekwisha kwa vile mitaala hii hata pale inapobadilishwa inalengwa zaidi kwa fikra za ukoloni mamboleo, inamuondolea mtu anayeipta elimu hiyo, uelewa wake wa kwamba yupo wapi, na utamaduni wake ukoje, je utaifa wake, je lugha yake, kwa nini yupo vile alivyo(Kama ni umaskini wa kutupwa).
Elimu yetu nchini na mitaala ya kimapokeo imewafanya wasomi wetu nchini kuwa ni wasomi wasiojiamini, wasiofikiri zaidi maendeleo ya nchi yao mbali na kujifikiria maslahi binafsi, hawana uhuru wa kuhoji mambo ya nchi yao, hawana hoja za fikra pevu juu ya serikali yao na hawana uwezo wa kujenga hoja, umoja juu ya kero zao zinazowakabili ndani ya jamii wanamoishi na kero za jamii ya watanzania. Hii labda ni kwa sababu ya elimu waliyonayo imewajenga kutofikiri na kutokuwa na fikra pevu ya kutafakari mambo.

Na hata pale baadhi ya wasomi wetu wanapojaribu sasa kuonesha hata juhudi binafsi za kujenga hoja na fikra pevu basi huhofia tena utawala na uongozi wa sehemu wanayotaka kuhoji kwa sababu tu inawezekana katika utawala, menejiment, uongozi wa sehemu husika nao ukawa haujiamini vile vile kwa vile una fikra zisizo pevu, na tuseme basi una elimu zilizojaa hofu ya kutoweza kujenga fikra pevu, basi ni kwa sababu hiyo ya mitaala ya kikoloni. Hapa uamuzi wa kimabavu, na vitisho huibuka bila kujenga hoja za kukabiliana na masuala yanayotakiwa ufumbuzi.

Je hapa tutasemaje wakati jinsi miaka inavyokwenda ndio jinsi ukondoo wa wasomi wetu unaongezeka na kuwa wakimya zaidi wa kufumbia macho kila kitu kinachotokea katika jamii ya watanzania. Hii imesababisha hata ndani ya jamii kundi la wanazuo wetu kudharaulika hata pale wanapokuwa na hoja za maana.
Kwa mfano migogoro katika vyuo vikuu vyetu nchini hasa pale panapotokea wanazuo hawa(wanafunzi) wanapojaribu kufuatilia maslahi yao ya kielimu katika miundo ya mitaala inavyoendeshwa vyuoni, maslahi yao ya jisni gani mazingira ya elimu yanavyotolewa vyuoni, basi moja kwa moja huonekana wahuni, wababaishaji, hasa pale wanapotumia njia za migomo na maandamano. Lakini vile vile tuelewe kwamba mtu kufikia hatua ya mgomo na kuandamana ujue hapo awali hakusikilizwa ndio maana akatumia njia hiyo ili jamii ya kitaifa na kimataifa iweze nayo kuelewa kwamba mtu huyu anahitaji kupata hiki.

Pamoja na usomi usiokuwa wa kujiamini kwa watanzania bado, usomi huo umeegemea kwenye lengo la kutafuta ajira pekee, na hapa siwezi kulaumu kwa vile mazingira ya kielimu yalivyotolewa kutokana na mitaala hiyo ilinaelekeza kwenye ajira zaidi kuliko kujitegemea. Kwani kama mitaala hiyo ni ya kikoloni, basi wakoloni waliweka mitaala hiyo ili uweze kuwa karani wao yaani mtumishi?, hawakuweka mitaala ya kuwa wewe mtanzania uweze kufikiri kujitemea(kujiajiri), hata kama una elimu yako ya uprofesa. Hilo silaumu sana ila tulifanya makosa tangu miaka hiyo ya 1961, baada ya kujitawala na bado tunaendelea kufanya makosa hayo. Bado hatulitambui hilo, ila tunaendelea kuhimiza eti wasomi wetu wasitegemee ajira pekee na wategemee elimu yao kujiajiri. Je swal, “hiyo elimu waliyoipata imewajenga katika kujitegemea(kujiajiri)”?, au ni elimu ya nadharia ya maneno tu isiyokuwa na nadharia ya vitendo.

Fikiria sasa elimu yetu, inakotupeleka na mitaala yetu, kilio kimeanza kutuumbua, maghorofa hayoo yameanza kuporomoka kwa sababu ya wahandisi wasio kuwa na fikra pevu juu ya uhandisi wao. Na inawezekana hata miataala inayotolewa katika uhandisi ni ile ile ya kikoloni bila kuzingatia mazingira yetu na jinsi ya kuwafanya wahandisi wetu wawe ni wahandisi wenye kujiamini na wenye fikra za ubunifu zaidi kuliko kutegema kanuni(formula) za vitabuni pekee wakati mazingira yetu ni mengine.

Utashangaa mwanafunzi wa uhandisi tena wa majengo anakuwa amejaa elimu ya nadharia ya darasani pekee huku nadharia ya vitendo ni mtupu, tena anaipata kwa wiki zisizozidi 6 au 8 tu kwa kila mwaka, hizo ni sawa na miezi 2 tu, ambapo, mwanafunzi huyo atakaa chuoni kwa miaka 4, miaka 3 yote huenda katika masomo kwa nadharia ya vitendo kwa wiki 6 au8, takribani miezi hiyo 2. Kwa hiyo uhandisi wake utakuwa umejaa nadharia ya vitendo wa miezi 6 tu katika miaka 4 ambapo ni miezi 48 katika shahada yake ya uhandisi majengo. Je kwa miezi hiyo 6 ya nadharia ya vitendo inamtosha mhitimu huyu wa uhandisi pale Mlimani kusimamia na kujenga jumba la ghorofa hata 2 tu kwa umahiri kabisa?.

Lakini hata hivyo, hapa serikali yenyewe hailioni hili, hata wale wanaowapika wahandisi wenyewe hawalioni hili. Je unafikiri tatizo hapa liko wapi?.

Basi na kwa vile mambo haya yote bado hayajafikirika kwa serikali yetu, na bado hata wasomi wetu wenye kuweza kuyang’amua haya hawajaweza kufanya hivi, basi fikra pevu kwa wasomi wetu ni ndoto isiyotafsirika kwa upesi pindi mtu anapostuka toka usingizini, tunahitaji nabii kama Daniel aweze kutafsri ndoto hii, na hatima ya muelekeo wa elimu yetu.